Charles Mhagama, Meya wa Manispaa ya Songea. |
Na Mwandishi
wetu,
Songea.
CHALRES Mhagama, ambaye ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma, ameburutwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi mfawidhi wilaya
ya Songea mkoani humo kwa kosa la kutoa rushwa, ikiwa ni lengo la kupora
kiwanja cha Ofisa mtendaji wa kata ya Matogoro.
Akisomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu, Elizabeth Missana na Mwendesha
mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Greigory Joseph
alisema mwaka 2010 katika kata hiyo, Mhagama alitoa shilingi 250,000 na kumpatia
Shaibu Ngonyani kama kishawishi cha kumwandikia mkataba feki wa mauziano ya
kiwanja hicho.
Mwendesha mshataka huyo aliendelea kudai Mahakamani hapo
kuwa, Mhagama alikuwa akitoa fedha hizo akiwa ni Diwani wa kata ya Matogoro
ambapo kosa la kutoa rushwa aliloshtakiwa nalo, ni kinyume na kifungu namba 15
kidogo 1B cha sheria ya uzuiaji na upambanaji wa rushwa namba 11 cha mwaka
2007.
Joseph aliieleza Mahakama kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika
na taasisi ipo tayari kuendelea na shauri hilo, ili sheria iweze kuchukua
mkondo wake.
Kesi hiyo ni jinai namba 38 ya mwaka 2015, ambapo mshtakiwa
amekana mashtaka yupo nje kwa dhamana ya maneno shilingi 250,000 na kwamba
itasikilizwa tena Aprili 16 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment