Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma,
kimesema kwamba walimu wake waliopo wilayani humo, wanaidai serikali shilingi
milioni 238,777,267.30 kwa muda mrefu sasa jambo ambalo linawafanya walimu
washindwe kuwajibika ipasavyo mashuleni.
Imeelezwa kuwa deni hilo ni la madai mbalimbali ambayo ni
malimbikizo, uhamisho, matibabu, likizo, masomo na kujikimu hivyo wameitaka
serikali kuhakikisha deni linalipwa mapema ili kuondoa malalamiko miongoni
mwao.
Hayo yalisemwa na Katibu mkuu wa CWT wilayani Mbinga, Werner Mhagama
alipokuwa akisoma taarifa ya utendaji kazi za chama kwa kipindi cha mwezi Julai
2013 hadi Disemba 2014 kwenye mkutano mkuu wa wilaya, uliofanyika ukumbi wa
Uvikambi uliopo mjini hapa.
Katibu huyo alieleza kuwa katika kipindi hiki, chama kimekuwa
na matatizo ya kutokuwa na maelewano, kati ya uongozi wa CWT na baadhi ya
viongozi wa wilaya hiyo hasa pale wanapofanya kazi ya ufuatiliaji wa madai
mbalimbali ya walimu.
Alisema ili walimu warudi na kufanya kazi kwa nguvu na ufasaha
zaidi, wanaiomba serikali kutoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri, kuteua
wasimamizi makini na kusambaza vifaa vya kutosha shuleni, kuendesha semina kwa
walimu ili kuboresha ufundishaji, wanasiasa kutoingilia masuala ya kitaaluma,
kuwapandisha vyeo na kuwalipa stahiki zao kwa wakati.
Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo ulifanyika
uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali ambao watakiongoza chama hicho
wilayani Mbinga, katika kipindi cha miaka mitano ambapo nafasi ya Mwenyekiti
alichaguliwa Batson Mpogolo aliyepata kura 156 na kuwabwaga wenzake watatu
ambao walikuwa wakiwania nafasi hiyo.
Aidha nafasi ya Mweka hazina ilikuwa ikigombewa na watu sita
na kwamba Grace Mbelle aliweza kuibuka kuwa mshindi baada ya kupata kura 97,
mwakilishi wa walimu wanawake wagombea walikuwa wawili ambapo Akwilina Ndipo
aliibuka mshindi kwa kura 197.
Vilevile Hekelius Ndunguru ambaye alikuwa akigombea nafasi ya
mwakilishi walimu walemavu aliweza kupata kura 162, ambapo nafasi mbili
wagombea walipita bila kupingwa ambazo ni mwakilishi wa uongozi taasisi za
elimu ilichukuliwa na Rogatus Mapunda kwa kura 252 na mwakilishi wa vyuo vya
maendeleo ya wananchi, Abraham Chimbuli alipata kura 250.
Mwakilishi kwa shule za msingi walitakiwa wapatikane watu
wanne ambapo ilichukuliwa na Marietha Komba aliyepata kura 69, January Kunani kura
48, Philotheus Mapunda kura 47 na Thomas Komba kura 28 na kwamba uwakilishi
shule za awali mshindi alikuwa Philotheus Mapunda kwa kura 75, walimu vijana
Gaudence Mbunda aliyepata kura 129 na wawakilishi wawili shule za sekondari
ilinyakuliwa na Frank Kinunda kwa kura 126 na Januari Turuka aliyeshinda kwa
kupata kura 127.
No comments:
Post a Comment