Na Steven Augustino,
Tunduru.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
kimetofautiana na tamko la vijana wa chama hicho, katika tarafa ya Matemanga
juu ya maamuzi yao ya kukishinikiza kumtawaza Omary Ajili Kalolo, kuwa
mgombea pekee kwa nafasi ya ubunge Jimbo la Tunduru Kaskazini kwenye uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hilo linakuja pia, kwa chama hicho kuwataka wabunge, madiwani
na viongozi wengine waliochaguliwa na wananchi kutimiza ahadi walizoahidi
wakati wa kampeni ya uchaguzi uliopita, ili kujiwekea akiba ya kuchaguliwa tena
vinginevyo wasitegemee kubebwa ili waweze, kushinda katika uchaguzi ujao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tunduru, Hamisi
Kaesa alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi, ambao walikusanyika na
kuhudhuria sherehe za ushindi wa chama hicho, katika kijiji cha Mtengashari kata
ya Ligunga wilayani hapa.
Akifafanua taarifa hiyo Kaesa, aliwataka pia makatibu wote wa
CCM na watendaji wengine ndani ya chama kuanzia ngazi ya tawi, shina na kata kupeleka
ofisini kwake majina ya wagombea watakaokubalika na wanachama wengi, vinginevyo
wao ndio watakaokuwa wa kwanza kuwajibishwa, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza
kazi.
“Mchakato utakapofikia wakati wake wagombea kujinadi, tendeni
haki kwa kupendekeza majina ya wagombea, wanaokubalika na wanachama wengi”,
alisema Kaesa.
Kaesa aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa viongozi,
ambao watapeleka mapendekezo yatakayotumia utaratibu wa kuchukua au kutumia,
maelekezo ya mtu mmoja mmoja kulingana na mapenzi ama nguvu ya fedha.
“Binafsi siwezi kuwa msemaji wa mgombea fulani, kati ya
wanachama ambao watatumia haki yao ya kikatiba, kuomba nafasi za uongozi kupitia
chama”, alisisitiza.
No comments:
Post a Comment