Na Julius Konala,
Songea.
MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Profesa Norman
Sigalla amewataka watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kumpa ushirikiano wa
kutosha, ikiwa ni lengo la kuimarisha utendaji kazi kwa manufaa ya jamii, na
upambanaji wa vita dhidi ya watu wenye tabia chafu ya kukatisha maendeleo ya wanafunzi
masomo darasani hususani kwa watoto wa kike, kuwapa ujauzito.
Sigalla alitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akizungumza na
watumishi wa kada mbalimbali, wakiwemo pia na wakuu wa idara wa halmashauri hiyo kwenye ukumbi wa mikutano
uliopo, ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kwa lengo la kufamihana.
Alisema hatakuwa na huruma wala kumfumbia macho, mtumishi yeyote
atakayebainika anaendesha vitendo viovu, huku akiapa kuwa hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yake, sambamba na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.
“Natoa onyo hata kwa wazazi na walezi, ambao watakabainika
kushindwa kutoa ushirikiano kwa serikali yetu katika kuwafichua watu ambao
wamewapa ujauzito watoto waliokatika wakati wa kwenda shule, kwa sababu ya
kurubuniwa na fedha au kitu fulani kwa lengo la kupoteza ushahidi, hatua kali
za kisheria zitachukuliwa dhidi yao”, alisema Sigalla.
Aidha amewataka watumishi hao wa halmashauri ya Songea, kutumia
muda mwingi kwa ajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo na kuwatumikia wananchi
badala ya muda mwingi kukaa na kupigana majungu, jambo ambalo amedai kuwa ni
adui mkubwa wa maendeleo katika halmashauri yoyote ile.
Vilevile kwa upande wa watumishi waliobahatika kuwa na elimu
na nyadhifa za juu, katika halmashauri hiyo waache tabia ya kujifanya miungu
watu kwa kunyanyasa na kudharau wenzao ambao wana elimu ndogo, kwa
madai kwamba wanapaswa kutambua kuwa kila mmoja anamchango na thamani yake
katika jamii.
Hata hivyo, Profesa Sigalla amehamishiwa katika wilaya ya
Songea mkoani Ruvuma, kuendelea na wadhifa wake wa kuwa mkuu wa wilaya hiyo
akitokea wilaya ya Mbeya baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko na uteuzi wa wakuu hao miezi michache
iliyopita.
No comments:
Post a Comment