Waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja. |
Na Kassian Nyandindi,
Aliyekuwa Mtwara.
MTANDAO wa kutetea haki za binadamu Tanzania (THRDC) umewataka waandishi wa habari nchini, kuzingatia usalama wa kazi zao pindi
wanapokuwa kazini ili kuweza kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza baadae,
hasa katika kipindi kijacho kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika,
Oktoba mwaka huu.
Imeelezwa kuwa mwaka huu ni mwaka ambao unahekaheka nyingi,
hivyo ni kipindi ambacho si salama kwa waandishi wa habari, na kwamba
wanakumbushwa kuzingatia usalama wa kazi zao kwa kutambua hatari, vitisho
pamoja na udhaifu katika usalama.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa THRDC, Onesmo Olengurumwa
kwenye mafunzo ya usalama na tathimini ya athari kwa watetezi ambayo yametolewa
kwa waandishi wa habari 28, toka nyanda za juu Kusini ambayo inajumuisha mikoa
ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Alisema kuwa kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu
ujao ni kipindi kigumu sana kwa waandishi wa habari, hivyo wanatakiwa kutambua
mazingira ya kufanyia kazi kutokana na kukabiliwa na hatari kubwa kipindi cha
kufanya kazi.
"Tunatambua ninyi ni waandishi wa habari ambao mnatoka
kwenye utajiri lakini watu wake ni maskini, kipindi cha uchaguzi kinakaribia
lazima mnapofanya kazi zenu mtambue kuna hatari, lakini pia kujiandaa katika
maswala ya usalama”, alisema.
Kwa upande wake mwanasheria wa THRDC, Benedict Ishabakaki
alisema kuwa vyombo vya habari visaidie waandishi wao pale wanapokwenda kwenye
matukio maalum, hasa ya kiuchunguzi katika kazi za kila siku.
Kwa upande wao waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo,
walisema kwa nyakti tofauti kwamba, kazi zao zinakabiliwa na changamoto nyingi
ambazo zinasababisha kushindwa kufanya kwa ufanisi mkubwa, hivyo wamewataka
wamiliki wa vyombo vya habari kujali maslahi ya waandishi wao, ili waweze
kufanya kazi ipasavyo.
No comments:
Post a Comment