Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre Baptiste Mapunda,
HISTORIA ya siasa duniani, haitengani sana na
historia ya dini. Vitu hivi
viwili kwa maisha ya mwanadamu, vimekuwa sambamba na vyenye mafao kwa
jamii yoyote ile duniani ambapo kwa upande mwingine dini na siasa vimeleta
matatizo makubwa hapa duniani.
Uhusiano mzuri usipojengwa kati ya siasa na dini, hakika katika
dunia hii na nchi yetu kwa ujumla tutaendelea kushuhudia machafuko na uharibifu
mkubwa wa mali, pamoja na mauti dhidi ya
binadamu kama yalivyowahi kutokea hapa nchini hasa katika kampeni za kisiasa.
Mara nyingi maovu hayo, yanasababishwa na uelewa mdogo juu ya mahusiano ya
siasa na dini.
Na hivi sasa Tanzania imezalisha ugonjwa mpya unaojulikana
kwa jina la “udini.” Unapoanza kuingiza udini katika ajira, elimu, afya na siasa ujue kwamba usalama wa nchi huenda ukawa hatarini.
Kutenganisha kabisa siasa na dini ni kitu ambacho hakiwezekani
katika dunia ya leo, bali kinachotafutwa ni kila taasisi kuielewa vyema inahusiana
vipi na nyingine, na kutengeneza mipaka yake na leo hii ndiyo ninaandika kwamba;
“siasa bila dini ni uwenda wazimu.”
Huwezi kusema wewe unashughulika na siasa, halafu
ukajidanganya kwamba hauhusiki na
masuala ya dini, wananchi wengi ni
waumini wa madhehebu mbalimbali mathalani kwa nchi ya Tanzania kuna waislamu,
wakristo, wabudha, wahindu, na hata wapagani.
Siasa ambayo haigusi maisha ya waumini, inakuwa imejitenga na
jamii husika na kitu muhimu na kinachotakiwa hapa, ni busara kujenga mahusiano
mazuri kati ya nyanja hizi mbili bila kuwepo njia potofu.
Katika siasa za Tanzania, nimegundua kuanzia kelele za muda
mrefu zinazotolewa na serikali, pamoja na wanasiasa kuwataka viongozi wa kiroho
au dini wasichanganye dini na siasa, hapa nasema hakuna msingi wowote ule kutokana
na mambo hayo mawili, hayawezi kutenganishwa kabisa.
Wanaoshikilia msimamo huo, wanaonyesha woga wa juu na uelewa
finyu katika masuala ya dini na siasa, hii ni bahati mbaya.
Kwa sisi wakristo tunasema, Yesu Kristo hakuhubiri habari za
ufalme wa Mungu tu na kuacha dhambi, bali aligusa maswala ya jamii kama amani,
umaskini, kutenda haki, mahusiano mazuri, madhara ya rushwa na ufisadi, wizi wa
mali ya umma, utunzaji wa rasilimali na
hata kuponya magonjwa na hii ndiyo injili sahihi yaani injili ya jamii.
Yesu alikuwa akihubiri injili ya jamii na sisi je haitupasi kuhubiri
injili hiyo hiyo ya jamii? Je, viongozi wa serikali na wanasiasa msingi wa hofu yao juu ya
viongozi wa kiroho, kuongelea masuala ya kisiasa katika nyumba za ibada ni nini?
Wiki jana kanisa katoliki, lilitoa msimamo wake kuhusiana na
kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini
Tanzania, kupitia tume ya haki na amani kwa ushirikiano na CPT wametoa waraka au tamko ikipendekeza
kusitishwa kwa mchkakato wa kura ya maoni, ili kupisha maandalizi mazuri ya uchaguzi
mkuu mwezi Oktoba mwaka huu, je hapo kanisa limefanya siasa?
Ni wajibu wa kanisa kama chombo cha wokovu kwa wanadamu wote,
na kiongozi wa imani na jamii kufanya kazi yake hii ya kinabii, sura ya nne ya
ujumbe wa Maaskofu katoliki wa kwaresma mwaka huu, ambapo nakala yake ninayo
hapa mezani unaongelea “wajibu wa kijamii wa kanisa”. Sehemu hii inasema kwamba;
kila mara kanisa linapotimiza wajibu huu linashutumiwa kuingilia siasa ambapo tafsiri
hiyo nasema ni potofu.
Kamwe kanisa katoliki haliwezi kukaa pembeni, kwani litakuwa
linafanya dhambi ya kutotimiza wajibu wake kwa jamii. Injili ya Yesu ambayo ni ya
upendo, amani na umoja lazima ihubiriwe kwa kila mtu katika jamii husika, kwa mfano Yesu
anafundisha tuache siasa za jino kwa jino.
Katika ujumbe huu wa kwaresima Baba wa Taifa, hayati Mwalimu
Julius Nyerere amenukuliwa kwamba aliwahi kuliasa kanisa akisema, “iwapo
kanisa halitashiriki kwa vitendo katika
maasi dhidi ya mifumo dhalimu ya kiuchumi inayosababisha watu, kutoswa katika
fedheha ya umaskini na kudhalilishwa, kanisa
halitakuwa na maana yeyote kwa watu na dini ya kikristo itapoteza mvuto na kuwa
kama ushirikina, jambo hili likitokea, kanisa litakufa.”
Katika jamii ya Kiyahudi enzi za kale, manabii walikuwa
wanaishi ikulu pamoja na mflame wao, kwa
lengo la kumsaidia mfalme katika kazi
yake ya kuongoza jamii. Ni nabii aliyekuwa
anampaka mafuta mfalme ili mkono wa Mungu, nguvu, na hekima iwe naye katika
kazi yake ya kuhudumia jamii nzima bila ubaguzi.
Tanzania ya leo inahitaji manabii, kama alivyojitokeaza Baba
wa Taifa Mwalimu Nyerere. Lakini pia ni wajibu mkuu wa viongozi wa dini
kuwasaidia viongozi wa serikali na wanasiasa ili waweze kuwa na roho ya Mungu
katika uongozi wao na ndiyo maana nasema, siasa bila dini ni uwenda wazimu.”
Ikumbukwe kuwa enzi za kale wakati wa uteuzi wa kiongozi wa
jamii, mtu aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo mara nyingi, alikuwa ni yule
aliyeonekana ni mcha-Mungu na watu walimuamini ataweza kuongoza vyema kwa
sababu, sauti ya Mungu ilikuwa ndani yake. Mimi naamini Nyerere alikuwa
kiongozi bora kwa sababu alikuwa pia na uchaji wa Mungu.
Kuipotosha jamii kwamba, viongozi wa dini hawana uhusiano na
mambo ya kisiasa ni kutowatendea haki ni lazima tutambue kwamba viongozi wa
dini ni viongozi wa jamii pia. Mimi ningependa kujua je, mpaka wa dini na siasa
upo wapi, ndiyo maana mimi naamini kwamba siasa bila dini ni uwenda wazimu
hivyo wananchi wanaohutubiwa katika mikutano ya kisiasa majukwaani siku ya
ibada wanakuwa waumini wetu.
Kutaka kuwatenganisha viongozi wa dini na siasa, ni kutaka
kujenga chuki kati ya waumini na viongozi wao, mwisho napendekeza kwamba
viongozi wa serikali na wanasiasa wa vyama vyote lazima waepuke kuwapotosha
waumini wetu, na kuwajenga chuki na viongozi wa madhehebu yao.
Mungu ibariki Afrika, Tanzania na watu wake.
Mwandishi wa makala haya anapatikana
kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment