Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. |
Na Kassian Nyandindi,
BUNDI ameendelea
kumsakama Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
Hussein Ngaga ambapo sasa ameingia katika kashfa mpya akidaiwa kuwaibia
wakulima wa kahawa wilayani humo, zaidi ya shilingi milioni 783,399,412 baada ya kahawa
yao kuuzwa mnadani Moshi.
Wakulima hao ni wale
ambao walikopeshwa fedha, shilingi bilioni 2 na Shirika la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) kupitia vyama vyao vya ushirika (AMCOS) vilivyopo wilayani humo, lengo
la fedha hizo kutolewa na shirika hilo lilikuwa ni kutoa mikopo yenye gharama
nafuu kwa wakulima wadogo wadogo, ambao wamejiunga kisheria katika vikundi
hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Hayo yamebainika
kufuatia uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, ambapo wakulima
kutoka vyama vinne vya ushirika Mahilo, Ngaka, Ngima na Pilikano ambao
hujishughulisha na uzalishaji wa zao la kahawa ndio walioibiwa fedha hizo.
Wizi huo unadhihirisha
pale mkurugenzi huyo, badala ya kuwalipa wakulima hao shilingi bilioni 4,104,748,612
yeye aliwalipa shilingi bilioni 3,321,349,200 na kuficha mwenendo mzima wa fomu
ya mauzo ya kahawa (Account Sell) ili wakulima hao wasiweze kujua juu ya ukweli
wa kahawa zao namna gani zilivyouzwa huko mnadani, jambo ambalo analalamikiwa
hadi sasa.
Gazeti hili limefanikiwa
kupata nakala ya fomu ya mauzo ya kahawa kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ambayo
inaonesha uhalisia wa mauzo yote ya jumla kwa kahawa zilizouzwa na vyama hivyo
vya ushirika msimu wa mwaka 2014/2015 hivyo inadhirisha wazi wakulima hao wameibiwa fedha
hizo, huku wengine wakisema wanaiomba serikali kuingilia kati ili waweze kupata
fedha zao.
Wakulima hao wamekuwa
wakimtaka kwa muda mrefu mkurugenzi huyo awapatie fomu hiyo ya mauzo ya kahawa,
lakini hadi leo hii hajawapatia na wamegonga mwamba.
Kadhalika habari
zilizopatikana kutoka kwenye vyanzo vyetu mbalimbali vinaeleza kuwa, hivi sasa baadhi
ya wakulima wanampango wa kwenda kuuona uongozi wa NSSF, ili wafikishe kilio
chao na kuwataka watume wakaguzi kwa ajili ya kukagua mwenendo wa matumizi ya
fedha hizo walizokopeshwa, huku wakidai kuwa katika mkopo huo kuna zaidi ya
shilingi milioni 300 zilibakia wakati wa mchakato wa manunuzi ya kahawa zao na hawajui
zimeenda wapi.
Walisema kuwa wananyimwa
hata kupewa fomu yenye kuonyesha mwenendo wa matumizi ya fedha hizo
walizokopeshwa katika akaunti zao za vyama vya ushirika (Bank Statement) ambazo
zilingizwa huko, ili waweze kujua zilitumikaje na hili linatokana na mkurugenzi
Ngaga kupangia matumizi fedha hizo na kuzuia viongozi wa AMCOS hizo
kutozifanyia matumizi wakati wa msimu wa manunuzi ya kahawa ulipofanyika, mpaka
ruhusa itoke kwake jambo ambalo limefafanuliwa kwamba ni ukiukwaji wa sheria na
taratibu za vyama vya ushirika.
Walifafanua kwamba kitendo
hicho kilichofanywa na mkurugenzi huyo amemdanganya Rais Jakaya Kikwete, kwa kauli
yake aliyoitoa hivi karibuni mbele yake kwamba fedha hizo watakabidhiwa
walengwa wa vyama hivyo na kukopeshana wenyewe, kwa mujibu wa taratibu husika
ili waweze kunufaika nazo na hatimaye waondokane na umasikini.
Rais Kikwete mnamo Julai
19 mwaka jana, alikabidhi mfano wa hundi kwa viongozi wa vyama hivyo vinne vya
ushirika wilayani Mbinga, ambavyo vilikopeshwa fedha hizo na shirika hilo
alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, mkurugenzi huyo
alimhakikishia Rais Kikwete mbele ya umma katika mkutano wa hadhara uliofanyika
stendi kuu ya magari ya abiria mjini hapa kwamba taratibu zitazingatiwa.
Mahilo, Ngaka, Ngima na
Pilikano ni vyama vya ushirika ambavyo hujishughulisha na uzalishaji wa zao la
kahawa wilayani hapa na kila kimoja kilipewa shilingi milioni 500 lakini
mkurugenzi Ngaga, alitengeneza utaratibu anaoujua yeye na kuvipatia fedha
kidogo kidogo kulingana na kiasi cha kahawa, inayoingizwa kiwandani kwa ajili
ya kukobolewa na ndio maana leo analalamikiwa.
Hata baadhi ya watumishi
wa halmashauri ya wilaya hiyo (majina tunayo) walionekana muda mwingi wakitumia
magari ya halmashauri kutia mafuta ambayo ilibidi yakafanye shughuli nyingine
za maendeleo ya wananchi vijijini, wakilipana posho na kufanya ufuatiliaji
kuhakikisha kwamba vikundi vinapeleka kahawa kiwandani ndipo vinakopeshwa fedha
hiyo, jambo ambalo watu wengi walikuwa wakihoji inakuwaje halmashauri inaingia
katika biashara ya kahawa?
Pia wakulima wa vyama
hivyo vya ushirika kwa nyakati tofauti, walidai kuwa huenda mkurugenzi huyo
alifanya hivyo akiwa na makusudi yake binafsi, ili fedha hizo aweze kunufaika
nazo kwa namna moja au nyingine na sio mkulima, kama shirika la NSSF
lilivyolenga.
Walidai kuwa pamoja na
fedha hizo kulenga kumpunguzia mkulima wa kahawa makali ya maisha, bado hawaoni
tofauti kama ilivyo kwa makampuni binafsi ambayo yalikuwa yakinunua kahawa
wilayani humo, kwa bei inayoridhisha.
Baadhi ya wakulima walio
katika vikundi ambao walikopeshwa fedha hizo wamesikitishwa na kitendo hicho,
huku wengine wakieleza kuwa wao wanachoelewa ni kwamba fedha hizo baada ya
kuingizwa kwenye akaunti za vyama vyao vya ushirika na wanachama kupitia viongozi
wao ilikuwa wajipangie utaratibu wao wenyewe wa kukopeshana kwa kuzingatia
taratibu na sheria za ushirika, kulingana na kiasi cha kahawa walichonacho na
sio utaratibu alioutumia mkurugenzi huyo kupangia matumizi wakati akijua fika
anavunja sheria au kukiuka taratibu husika.
Lengo la NSSF kuwakopesha
wakulima fedha hizo, lilikuwa waondokane na changamnoto ya kukosa uhakika wa
huduma za afya, ununuaji wa pembejeo ili waongeze uzalishaji na uhakika wa
kipato baada ya kufikia umri wa uzee, ambapo husababisha kushindwa kuendelea na
shughuli za kilimo.
Jitihada ya kumpata
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ngaga ofisini kwake ili
aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko haya hazikufanikiwa na simu yake ya
kiganjani ilikuwa haipatikani.
No comments:
Post a Comment