Friday, March 20, 2015

MFUKO WA BIMA YA AFYA WASHUSHA LAWAMA KWA WATENDAJI WA SERIKALI

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo, wakifuatilia hoja mbalimbali kwa umakini.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

IMEELEZWA kuwa mkoa wa Ruvuma, umekuwa ukikosa shilingi milioni 250 kila mwaka, kutokana na kuanzishwa utaratibu wa kutoa huduma za matibabu kupitia mfuko wa bima ya Afya ya jamii (NHIF) endapo viongozi wa halmashauri za mkoa huo wangeomba kupatiwa dawa kupitia mfumo huo, huku hali imetokana na kuwepo kwa michango ya wanachi kutoka katika kaya 26,058 ambazo huchangia fedha zao, huku wakikosa huduma waliyokusudia kuipata.

Meneja wa mfuko huo wa bima ya afya ya jamii mkoani Ruvuma, Slively Mgonza alisema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya mfuko huo, katika mkutano wa tathimini ya elimu, uliofanyika kimkoa katika ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya mlingoti, wilayani Tunduru mkoani humo.

“Nikituko cha ajabu, kwani endapo wangeomba fedha hizo zingesaidia kuondoa matatizo mbalimbali yanayozikabili hospitali, vituo vya afya  na zahanati katika utoaji wa huduma kwa jamii”, alisema Mgonza. 

Kwamujibu wa Mgonza, kati ya fedha hizo shilingi milioni 48  zilichangwa kutoka katika kaya 4,882 katika Manispaa ya Songea, milioni 56 kutoka katika kaya 5,699 zilizopo halmashauri ya wilaya songea na milioni 77 katika kaya 7,782 zilizopo Halmashauri ya wilaya ya Tunduru.


Alifafanua kuwa mfuko huo pia, katika kipindi hicho ulipokea kiasi cha shilingi milioni 35 kutoka katika kaya 3,510 zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, ambapo shilingi milioni 32 zilitoka katika kaya 3,27 zilizopo wilaya ya Mbinga na milioni 9 zilizoripotiwa kuchangwa na wananchi kutoka katika kaya  915 wilayani Nyasa.

Akitoa taarifa ya huduma ya mikopo ambayo pia imekuwa ikitolewa na mfuko huo,  kwa lengo la kuboresha ufanisi wa upatikanaji wa huduma za afya, Meneja huyo wa bima ya Afya ya jamii alisema, kinacho mshangaza zaidi ni kuona wadau hao kutokwenda kuomba mikopo hiyo na kufanya fursa hiyo kupotea bila manufaa yaliyolengwa na mfuko. 

Fursa hiyo ya mikopo alielezea kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 shirika hilo limetenga jumla ya shilingi bilioni 16 ambapo kati yake shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kukopesha vifaa tenganishi na bilioni 6 kwa ajili ya shughuli za ukarabati.

Mgonza aliendelea kufafanua kuwa, kutokana na uvivu wa watendaji katika halmashauri wamekuwa hawajishughulishi na uandikaji wa maombi hayo, jambo ambalo limeifanya bima ya afya kukopesha kwa chini ya asilimia 2 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo.

Awali akizungumza kwa niaba ya serikali, mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alizitaka halmashauri zilizopo mkoni humo, kutumia fursa zinazotolewa na mfuko huo ili wananchi waweze kuondokana na hatari ya kupoteza maisha yao  kutokana na kukosa huduma za afya. 

“Hivi sasa bima ya afya wameanzisha utaratibu wa kukopesha vifaa tenganishi, mikopo ya fedha za ukarabati wa majengo ya vituo vya afya, zahanati na hospitali tumieni fursa hii kuweza kuboresha maisha ya wananchi wetu”, alisisitiza.

Aidha katika taarifa hiyo Mwambungu, aliwataka wananchi kuondokana na dhana kuwa huduma ya bima ya afya inatolewa kwa wafanya kazi wa serikali pekee bali ni wananchi wote hivyo wanapaswa nao kujiunga.

Pia aliagiza viongozi wa mkoa huo, kufanya uhamasishaji wa kutosha kwa wananchi wao ili kuwawezesha kujiunga katika mfuko huo, hali ambayo itawafanya wawe na uhakika wa kupata matibabu pale wanapougua.

Katika kujenga msisitizo mkuu huyo wa mkoa, akatumia nafasi hiyo kwa kutoa tamko lenye amri ya kupata taarifa kwa wilaya zote ndani ya mkoa huo, ziwe zimekwisha kamilisha taratibu za kukopa fedha hizo katika kipindi cha miezi 6 ijayo, ili kuona fedha hizo zinakopwa na kuanza kuwasaidia wananchi.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Manispaa ya Songea Charles Mhagama na mwenyekiti wa halmashauri ya  wilaya ya Tunduru, Faridu Khamisi na wa wilaya ya Namtumbo, Steven Nana walisema wananchi wamekuwa wakisita kuchangia fedha kupitia mpango huo, kutokana na hospitali za serikali kutokuwa na uhakika na utaratibu mzuri, katika utekelezaji wa utoa huduma kwa jamii ambapo wakati mwingine hata dawa za matibabu imekuwa ni tatizo kupatikana pale mgonjwa anapohitaji matibabu.

No comments: