Na Amon Mtega,
Songea.
CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Songea
mkoani Ruvuma, kimeutaka uongozi wa Manispaa hiyo kushughulikia matatizo ya
walimu, ikiwemo kuwapandisha madaraja kwa wakati wale wote wanaostahili ili
kuondoa malalamiko kwa baadhi yao, ambao ni muda mrefu sasa umepita hawajapandishwa.
Mwenyekiti wa CWT katika tawi hilo, Mathias
Mwanjisi alitoa rai hiyo juzi alipokuwa kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi
viongozi wa chama hicho, akieleza kuwa licha ya wengi wao kuwa na vigezo
vinavyostahili kupandishwa madaraja lakini hakuna kilichotekelezwa hadi sasa.
Kadhalika Mwanjisi ambaye alikuwa akitetea
nafasi yake ya uenyekiti katika chama hicho, aliweza kushinda kwa kupata kura
84 huku mpinzani wake Edimund Nditi akipata kura 18 huku idadi ya wapiga kura wote
ilikuwa 102.
Matokeo hayo yalitangazwa na msimamizi mkuu wa
uchaguzi huo, Efigenia Nzota ambapo alitetea nafasi yake hiyo na mafanikio
yake alisema kuwa changamoto kubwa ni kwa baadhi ya walimu, ambao wanastahili
kupandishwa madaraja kushindwa kufanyiwa hivyo kwa wakati na hatimaye
kutengeneza malalamiko dhidi yao.
Alisema kuwa ili kuondoa dhana hiyo ya
malalamiko ni lazima viongozi wa kitengo husika cha Manispaa ya Songea, kupeleka
taarifa zote za walimu wanao stahili kupanda madaraja katika ofisi husika za
makao makuu na kufanyiwa kazi kwa haraka.
Mwenyekiti huyo akitoa neno la shukrani
kwa wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa uchaguzi, alisema kazi kubwa ni
kushikamana na kukijenga chama kwa kuepusha migogoro ambayo inaweza kuwagawa
bila sababu za msingi.
“Naomba tushikamane kukijenga chama chetu, tusiposhikamana
tutakiharibu chama na matokeo yake chama kitaingia kwenye migogoro ambayo
inaweza ikatugharimu baadaye, jambo ambalo siyo jema mbele ya jami”, alisema.
Hata hivyo katika uchaguzi huo nafasi mbalimbali
ziligombewa ikiwemo ya mweka hazina ambapo Emmnuel Kayuza alipita bila kupingwa,
kutokana na mpinzani wake Ananias Mbilinyi kujitoa mapema huku nafasi ya
uwakilishi walimu wanawake aliibuka kidedea, Sophia Luoga ambaye aliwabwaga
wapinzani wake watano.
No comments:
Post a Comment