Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre
Baptiste Mapunda,
KWANZA ni
lazima ieleweke kwamba, Wakristo kupitia Maaskofu wao hawaipingi Mahakama ya kadhi kama mahakama ya kadhi, ila
wanachopinga ni uanzishwaji kwa mamlaka ya serikali.
Swali ni kwa
nini serikali ijishughulishe na mahakama ya dini, wakati katiba imekataa?
Watanzania wengi wanajiuliza kuna agenda
gani ya siri iliyopo nyuma ya hii
mahakama? Kwa mantiki hiyo na kwa kuzingatia tamko la Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo na sababu nzito iliyotolewa, wakristo tujiandae kuipigia kura ya hapana katiba mpya kama tulivyoelekezwa na
wala siyo kulazimisha kama wengine wanavyotafsiri tamko hilo.
Toka kuundwa
kwa taifa letu la Tanganyika-Tanzania nchi yetu inajulikana kwamba serikali
yake si ya kidini ila wananchi wake wanadini. Katiba ya mwaka 1977 inatamka
hivyo na kila mtu anajua na hivyo basi masuala yote ya kidini yanapaswa kuendeshwa na dini husika.
Waumini wa
imani tofauti mathalani Wakristo na Waislamu, walikuwa wamekaa kwa amani hadi
miaka ya 90 katika kipindi cha Rais wa
awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi maarufu kama mzee wa “Ruksa” ndipo choko choko
za kidini zilipoanza kujitokeza.
Choko choko
hizi ziliambatana na madai kwamba, Waislamu walikuwa wanaonewa, kunyanyaswa na
kubaguliwa chini ya mfumo wa kikristo.
Kikaja kipindi
cha Benjamini Mkapa madai yalijitokeza,
lakini yeye alifuata katiba ya nchi hivi hakuweza kuyapa nafasi hata ya
kujadiliwa bungeni. Lakini leo cha ajabu ni kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ililiweka suala la mahakama ya kadhi katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka
1995.
Kuanzia hapo
basi Waislamu nchini, wameendelea na madai yao ya kubaguliwa kwa misingi kwamba
nchi inaendeshwa kwa “mfumo wa kikristo” sielewi hata maana yake ni nini.
Rais Kikwete
yeye anajitetea anasema siyo yeye aliyeliweka katika ilani ya uchaguzi ya mwaka l995, kwani yeye
hakuhusika katika utengenezaji wa ilani hiyo. Je madai hayo ni ya kweli?
Maaskofu wa
madhehebu ya kikristo wameshamwambia bayana
Rais Kikwete kwamba suala hilo ni la kiimani na hivi halifai kuingizwa
katika katiba na wala halitawezekana. Lakini bado serikali ya Rais Kikwete inaendelea kulipigania kiaina aina. Sasa
limeingizwa katika agenda ya katiba mpya, swali je, Rais Kikwete atafanikiwa kuwapatia Waislamu mahakama ya kadhi kabla hajaondoka ikulu?
Kwa upande wangu
naliona suala la mahakama ya kadhi ni kama sehemu ya utekelezaji wa Tamko la
Abuja la mwaka 1990 juu ya ustawi wa dini ya Kiislamu barani Afrika. Inasemekana lengo mojawapo kubwa la tamko hilo, ni kufuta
imani zisizo za kiislamu barani Afrika katika nchi wanachama na hivi kuanzisha
dola ya kiislamu itakayotawala kwa kutumia sharia.
Kama kuna mtu
anabisha juu ya hili basi aende tu kusearch katika mitandao, “ABUJA DECLARATION” na
atembelee
http//eaclj.org/component/content/article 25-religion-feature-article/…
atapata elimu kubwa sana juu ya jambo hili.
Suala la
mahakama ya kadhi hata kama linawahusu waislamu tu katika ndoa na mirathi
linabaki kuwa la kidini (imani). Bunge la katiba linapata wapi mamlaka ya
kulijadili jambo la kidini wakati katiba yetu imesema mambo ya dini yatakuwa
nje ya katiba? Je, bunge letu sasa limegeuka la kidini? Hawa Maaskofu na
wachungaji waliomo katika bunge hili
wanajisikiaje juu ya suala hili?
Kwa kweli hii
ni alama kwamba kama vile Mungu alivyoufanya moyo wa Farao ukawa mgumu,
basi hata leo anaendelea kumpa Rais Kikwete na serikali
yake ya CCM ugumu wa kuelewa na hivi
mwishowe Mungu atashinda tu. Spika wa Bunge la katiba anasema ameunda kamati ya
watu kumi kuangalia suala la mahakama ya kadhi je, wataliangalia kwa misingi
ipi? Sasa ni wazi kwamba Bunge hili limepotoka vibaya sana na hivi linapaswa
kusitishwa haraka sana.
Serikali ya
CCM na Rais Kikwete lazima ijiepushe na kujihusisha na masuala ya
kidini ndani ya Bunge la katiba na katika maeneo mengine, nasema hivi kwa
sababu hii ni kinyume cha sheria kabisa na serikali inajua hilo. Rais Kikwete
hachoki bado anaendelea kulipigania
suala hilo ingawaje anajificha asionekane lakini kwa sababu ni suala linalohusu
haki kwa dini nyingine, suala hili na
mipango yote ya siri inajulikana. Kwa Mungu hakuna siri yeyote ile kuna siku itafumuka tu.
Nataka kuihakikishia serikali ya CCM kwamba mpango
huu hautafanikiwa kamwe katika nchi hii na ukifanikiwa kitakuwa chanzo kikubwa
sana cha machafuko katika nchi, huu ni utabiri wangu. Ninawasihi wanaCCM
kuachana na mpango huu mara moja kwani tutaomba
usiku na mchana na Mungu atasikia tu. Kama CCM ina uwingi wa wabunge
katika nchi hii, basi sisi Wakristo tuna uwingi wa maaskofu, mapadre, wachungaji, wainjilisti, makatekista na waumini na
hata vichaa na wavuta bangi wataunga mkono jitihada zetu serikali ya CCM lazima
ijue haiwezi kushindana na nguvu za Mungu iulize Kenya kilitokea nini?
Mpango wa
kuifanya Tanzania nchi ya Kiislamu kwa
njama za mahakama ya kadhi umechelewa. Tunaungana
na Maskofu na viongozi wote wa kikristo
walioshauri tayari kwamba mahakama ya kadhi ianzishwe nje ya katiba,
kama yalivyo mahakama ya kanisa katoliki na madhehebu mengine. Kwa nini
kutafuta nguvu ya katiba? Je, watu
wakishawishika kutumia mahakama
ya kadhi vibaya itakuwaje? Mahakama ya kadhi haina maslahi kwa Watanzania labda Mashekhe wachache.
Hata ndani ya
waislamu wenyewe, mahakama ya kadhi
italeta mgawanyiko kati ya Bakwata na
Ansar Sunnar. Hawa ni wale wanaoendesha shuura ya Maimam wakiwa na ushawishi
mkubwa katika jamii ya waislamu wakisaidiwa na vyombo vyao vya mawasiliano kama
Radio Imani, Times FM, na gazeti la
An-Nuur na Nasaha.
Suala la mahakama
ya kadhi inaonekana ni la kimaslahi zaidi yaani; ajira kwa wachache. Lakini
swali la msingi ni hili, je watalipwa na
fedha za nani? Kama mahakimu na watendaji wa mahakama za kadhi watalipwa na
fedha za walipakodi yaani Watanzania wote basi huu ni unyanyasaji na ubaguzi
ambao unageuka kuwa udini na wala si haki kwa madhehebu mengine.
Ili kuleta usawa kwa dini zote na kwa sababu serikali ina pesa nyingi basi kila dini iingize mahakama zake ndani ya
katiba na watendaji wake walipwe, namna nyingine halitawezekana. Hivi
itawezekana vipi Wakristo wakubali mahakama za kadhi zitoe ajira kwa Waislamu
kuanzia ofisi ya Mtaa, Kata, tarafa, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa malipo ya pesa
ya walipa kodi wa Tanzania wakiwamo Wakristo. Hii ni haki kweli?
Wakristo wote wa Bara na Zanzibari wanahaki ya
kupinga mahakama ya kadhi (MK). Kuna uvumi kwamba maoni ya katiba mpya juu ya
mahakama ya kadhi yamechakachuliwa
kasoro Mbeya na Mwanza. Sasa najiuliza hivi mkoa wa Ruvuma Wakristo ndiyo
walioipitisha mahakama ya kadhi au
ni nani maana idadi ya Waislamu mkoani Ruvuma ni ndogo sana, ukilinganisha na
ya Wakristo.
Wanaodai uwepo
wa ubalozi wa Vatikani nchini, kwamba ni kinyume cha katiba basi hawaelewi
kitu. Ni vyema serikali ikalitolea jambo hili maelezo ya kina bila kuogopa
kundi lolote lile na kuonyesha wazi kwamba, ubalozi huo unaendeshwa kwa pesa ya
Wakatoliki na si pesa ya umma.
Ni upendeleo
serikali kutumia pesa ya walipakodi kwa masilahi ya dini moja, suala la
mahakama ya kadhi litaleta mgogoro wa kidini na machafuko nchini kama ilivyotokea
katika suala la “nani ana haki na mamlaka ya kuchinja.” Namna nyingine Wakristo
wote tutaungana ili kuikataa katiba mpya kwa sababu imebeba masilahi ya dini
moja.
Mwandishi wa
makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment