Na Julius
Konala,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa kutokamilika kwa wakati, ujenzi mradi wa maji
Kihongo uliopo katika kijiji cha Kihongo, kata ya Mapera wilayani Mbinga mkoa
wa Ruvuma, unatokana na ukosefu wa fedha hivyo serikali imeombwa kutekeleza
hilo ili mradi huo, uweze kujengwa kwa haraka na wananchi waweze kuondokana na
adha ya ukosefu wa maji.
Hayo yalisemwa kupitia taarifa fupi iliyosomwa na Afisa
mtendaji wa kijiji cha Kihongo, Danstan Hyera kwenye maadhimisho ya kilele cha
wiki ya maji yaliyofanyika kimkoa katika kijiji hicho wilayani Mbinga.
Aidha Hyera alisema kuwa, hivi sasa hata kazi za ujenzi
zimesimama hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuona umuhimu wa kuwezesha mradi
huo uweze kukamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma bora ya maji.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi mkuu wa wilaya hiyo,
Senyi Ngaga ambaye alikuwa akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu
aliwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuacha kuharibu mazingira ili
kuepukana na ukame unaoweza kujitokeza baadaye baada ya mazingira hayo
kuharibiwa.
Ngaga alieleza kuwa vitendo vya ukataji miti, kulima kwenye
vyanzo vya maji na uchomaji moto wakati wa kiangazi ni mambo ambayo ni adui wa
mazingira, yanapaswa kukemewa wakati wote ambapo wananchi wanapaswa pia kupewa
elimu mara kwa mara juu ya hilo, ili
waweze kuachana navyo.
“Natoa wito kwa wananchi wote wa wilaya hii, tuache tabia ya kukata
miti hovyo na kuchoma moto misitu wakati wa kiangazi, ikiwemo hata kulimna
kwenye vyanzo maji endapo hatutazingatia haya tutakaribisha ukame na kufanya
shughuli nyingi za kimaendeleo zishindwe kusonga mbele kutokana na kukosa
maji”, alisema.
Kadhalika Ngaga aliweza kuweka jiwe la msingi katika ujenzi mradi
wa maji wa wananchi wa kijiji hicho cha Kihongo, ambapo hadi kukamilika kwake
utagharimu kiasi cha shilingi milioni 827,329,140.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, alitumia pia fursa hiyo
kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika
daftari la wapiga kura, mara zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa katika wilaya
hiyo.
Pamoja na mambo mengine, naye Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka
ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) Salvatory Mugarula alisema ili
kuziwezesha taasisi za umma kutoa huduma bora kwa raia na wateja wake, kuna
kila sababu kwa taasisi kuzingatia viwango na ubora wa huduma ili kuondoa
malalamiko yasiyokuwa ya lazima, miongoni mwa jamii.
No comments:
Post a Comment