Na Amon Mtega,
Songea.
WATANZANIA wakati wote wa maisha yao ya kila siku, wametakiwa
kuishi kwa kuzingatia sheria zilizowekwa, ili kuepusha migogoro ambayo inaweza
kujitokeza baadaye katika jamii hasa pale inapotokea kundi moja au jingine, hukiuka
taratibu na kutozingatia miongozo ya sheria.
Naibu Askofu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Padre Camillius
Haulle alitoa rai hiyo alipokuwa kwenye sherehe ya kuwaaga wahitimu wa mafunzo
ya msaada wa kisheria (Paralegle) yaliyofanyika katika kituo cha kisheria cha, African Institute for Comparative
and International Law (AICL) kilichopo Mahenge mjini hapa.
Haulle alisema kuwa kama watanzania watatambua umuhimu huo,
huenda hata migogoro ambayo hujitokeza mara kwa mara katika jamii ikapungua au kwisha kabisa na kulifanya taifa, kuwa na watu ambao ni mfano bora mbele ya mataifa mengine.
Alisema, nchi yeyote ambayo watu wake wanaishi bila kuzingatia
sheria ambazo zimewekwa kwa mujibu wa taratibu husika, ni lazima kutakuwa na
machafuko makubwa kutokana na kila mmoja kutaka kutumia mabavu kulingana na
nafasi aliyonayo.
“Ndugu zangu sheria ni kama mlango ambao unazuia kutoka au
kuingia, bali kuwepo na sababu zinazoufanya ufunguliwe au ufungwe, hivyo ndiyo
inavyotakiwa Mtanzania aishi kwa kuzingatia haya”, alisema Askofu
Camillius.
Anna ambaye pia ni Mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto mkoani Ruvuma, alibainisha kuwa uwepo wa migogoro mingi ndani ya jamii, hasa kwa watu wa ndoa husababisha kuyumbisha familia zao na kuzifanya zishindwe kusonga mbele kimaendeleo.
Mwenyekiti huyo alikuwa mgeni rasmi katika sherehe
hizo, aliongeza kuwa hivi sasa kumekuwepo na wimbi la baadhi ya mabinti, kutoa
mimba na kuvitupa vichanga, huku akiitaka jamii kuachana na vitendo hivyo na endapo
wahitimu hao watafanya kazi ya kutoa msaada wa kisheria juu ya madhara
yanayoweza kujitokeza baadaye, hakika jamii itabadilika na hatimaye kuweza
kuondokana na hali hiyo.
No comments:
Post a Comment