Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KUTOKUWEPO kwa
matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Albino mkoani Ruvuma, wananchi
wa mkoa huo wameendelea kulaani vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya kundi hilo
tete, ambavyo vimekuwa vikiendelea kujitokeza katika maeneo ya kanda ya ziwa
hapa nchini.
Akizungumza na
waandishi wa habari mjini hapa, Katibu msaidizi wa chama cha watu wenye ulemavu
wa ngozi mkoani hapa, Fatuma Jumbe alisema kundi hilo la watu wenye ulemavu wa
ngozi linahitaji uangalizi wa hali ya juu na kuitaka serikali, kuweka mikakati
madhubuti ambayo itaweza kufanikisha katika kupambana na kuwakamata watu wenye
kushiriki kwa namna moja au nyingine kuua albino.
Lakini alipongeza
uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kukutana na
wawakilishi wa kundi hilo, pamoja na kuahidi kuunda tume ya kushughulikia
vitendo hivyo vya kikatili, dhidi ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi.
Fatuma alieleza kuwa
vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya kundi hilo, ambalo limekuwa likiishi kwa
hofu kubwa dhidi ya vitendo viovu wanavyofanyiwa linaleta wasiwasi hata kwa
makundi mengine ya walemavu, ambayo alishauri pia nayo yawe katika uangalizi mkubwa
na sio kungojea mpaka pale tatizo linapotokea ndipo hatua zichukuliwe.
“Hali hii kadiri siku
zinavyozidi kusonga mbele, tunajikuta tupo katika wakati mgumu sana, sijui
tufanyeje lakini tunazidi kuomba Mungu atuepushe na majanga haya”, alisema.
Naye, Prisela Chales
mwanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Songea ambaye ni mlemavu wa ngozi,
alisema kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo kunawatia hofu wao na kuwakatisha
tamaa ya kuendelea na masomo kwa kutojua hatima yao hasa pale wanapoamka mapema
alfajiri, kwa ajili ya kuelekea shuleni kuhudhuria masomo darasani.
Naye makamu mkuu wa
shule ya sekondari ya wasichana Songea, Winna Likiliwike akizungumzia hali hiyo
alifafanua kuwa shule yake ina watoto wenye ulemavu wa ngozi na vitendo hivyo,
ambavyo vinaendelea kufanyika hasa maeneo ya kanda ya ziwa vimekuwa vikiathiri
wanafunzi wake katika kuhudhuria masomo.
Ameziomba mamlaka
husika kufikia hatua ya kuchukua maamuzi magumu, dhidi ya wahusika ambao
wamekuwa wakithubutu kukata viungo vya watu wenye ulemavu na hata kukatisha
maisha ya watu wa kundi hilo, ni vyema nao wakaadhibiwa kulingana na kosa hilo
kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Mkuu wa mkoa wa
Ruvuma, Said Mwambungu akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya
wanawake duniani, kilichofanyika hivi karibuni kijiji cha Mpitimbi B wilayani
Songea, alisema serikali mkoani Ruvuma haitamvulia mtu yeyote atakayetajwa
kuhusika na vitendo hivyo vya ukatili hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa
haraka iwezekanavyo.
Mwambungu aliongeza
kuwa kundi hilo lenye ulemavu wa ngozi, lina haki sawa ya kuishi na hakuna mtu
yeyote mwenye haki ya kukata kiungo chochote cha binadamu mwenzake, au kukatisha
uhai wake kwa lengo la kujipatia kipato sasa ni lazima sheria ichukue mkondo
wake na huku akiziagiza mamlaka zote kuanzia ngazi ya familia mpaka mkoa,
kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya namna hiyo ambavyo vitaweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment