Rais Jakaya Kikwete. |
Na Kassian
Nyandindi,
AGIZO lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Jakaya Kikwete juu ya kutoondolewa kwa vifaa vya thamani katika shule
ya sekondari ya wasichana Mbinga mkoani Ruvuma, limepuuzwa na vifaa husika
vimeendolewa katika majengo ya shule hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein
Ngaga ndiye anayenyoshewa kidole kutumia nguvu kwa cheo alichonacho na kuchukua
vifaa hivyo huku akijua fika, Rais Kikwete alikwisha toa agizo vitu vilivyomo
ndani ya majengo ya shule hiyo visiondolewe.
Hivi karibuni, Rais Kikwete mnamo Julai 19 mwaka 2014 alikuwa
katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga, ambapo alitoa agizo hilo akilenga vifaa
hivyo viweze kuwasaidia walimu na wanafunzi ambao wanasoma katika shule hiyo.
Kitendo hicho kilichofanywa na Mkurugenzi wa wilaya hiyo,
kimeelezwa kuwa ni wizi na kudharau agizo la mkuu wake wa nchi, hivyo anapaswa
kuchukuliwa hatua ikiwemo kurudisha mali alizochukua, ili iwe fundisho kwa
viongozi wengine wenye tabia ya kupora mali za umma kwa kutumia nguvu.
Aidha imeelezwa kuwa hakuna kikao chochote kilichoketi na
kuridhia achukue mali za shule hiyo, ambavyo ni vifaa vya thamani
walivyokabidhiwa na mkandarasi wa ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka
pacha ya Peramiho hadi Mbinga mjini, jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko
miongoni mwa jamii.
Ngaga ananyoshewa kidole kwamba ametumia nguvu, na
kulazimisha kuchukua vifaa hivyo ambavyo wananchi wa kijiji cha Kigonsera kata
ya Kigonsera wilayani humo, walikabidhiwa na mfuko wa barabara wa Millenium
Challenge Account (MCA – Tanzania) mara baada ya Mkandarasi, ambaye ni kampuni
ya kichina ya Sinohydro Corporation Limited kukamilisha kazi ya ujenzi wa
barabara hiyo.
Mkandarasi huyo ambaye alikuwa ameingia mkataba na kijiji hicho
(nakala tunayo) inaonesha na kuthibitisha kuwa alikuwa ametumia sehemu ya ardhi
ya kijiji, kwa ajili ya kuweka kambi na kujenga majengo ambayo yalikuwa
yakitumika kulala wataalamu wa ujenzi wa barabara hiyo.
Hivyo mara baada ya kukamilisha kazi ya ujenzi, majengo na
mali kadhaa zilizomo ndani yake mnamo Januari 15 mwaka 2014 walikabidhiwa
kijiji, mbele ya kikao cha baraza la kata (WDC) kwa ajili ya matumizi ya shule ya
sekondari Kiamili iliyopo kijijini hapo wilayani humo, ili viweze kuwasaidia
walimu wanaofundisha shuleni hapo.
Mkurugenzi Ngaga kwa siku zilizofuata, alimtuma Ofisa utumishi
wake wa wilaya ya Mbinga, Emmanuel Kapinga kwenda kuchukua vitu vya thamani
vilivyomo ndani ya majengo hayo, kwa kutumia nguvu bila wananchi wa eneo hilo
kujulishwa kupitia vikao halali kitendo ambacho wanasema ni wizi, huku akijua
fika mali alizochukua ni za wananchi wa kijiji cha Kigonsera.
Ofisa utumishi huyo baada ya kuwasili katika eneo hilo,
anadaiwa kulazimisha kupewa funguo za majengo hayo ambazo zilikuwa zikitunzwa
na uongozi husika uliokabidhiwa mali hizo, na alipopewa aliingia ndani ya
majengo na kuchukua vitu kadhaa vilivyomo ndani yake na kuondoka navyo.
Mwandishi wetu baada ya kufanya ufuatiliaji wa kina juu ya
vitu hivyo vimepelekwa wapi, imebainika kuwa wamegawana vigogo kadhaa wa wilaya
ya Mbinga (majina tunayo) na kwenda kuvitumia majumbani kwao, ndio maana leo
kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale.
Hata baadhi ya madereva wa halmashauri ya wilaya hiyo, ambao
walishiriki katika mchakato wa kwenda kubeba vitu hivyo, nao walipewa chapuo la
kugawiwa baadhi ya vitu kama vile mitungi ya gesi.
No comments:
Post a Comment