Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKATI serikali ikiwataka viongozi wake katika
Halmashauri mbalimbali hapa nchini kufanya kazi kwa uwazi na kufuata taratibu
husika, hali hiyo imekuwa kinyume kwa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo
inadhihirisha pale agizo lililotolewa na Kaimu Afisa elimu msingi wa wilaya
hiyo, Alphonce Mwamwile juu ya michango wanayochanga wazazi kwa ajili ya
kuendeshea mitihani ya kata na shule mwishoni mwa mwezi na kuingizwa kwenye
akaunti ya Rukwa Computer Training Centre, imezua mapya kufuatia baadhi ya
Madiwani na Wenyeviti wa shule za msingi wa wilaya hiyo, kudai kuwa hakuna
kikao kilichoketi na kujenga makubaliano kwamba fedha hizo zipelekwe huko.
Madiwani na wenyeviti hao walidai kwa nyakati
tofauti kuwa, hata mchakato wa zabuni haujafanywa juu ya kumpata mzabuni huyo
ambaye hafahamiki ni wa kutoka mkoa au wilaya gani na amepewa jukumu la kuchapa
mitihani ya watoto wao, badala yake wanashangaa kuona waratibu elimu kata na
walimu wakuu mashuleni wakiagizwa kukusanya michango hiyo na kuiingiza kwenye
jina la akaunti hiyo.
Imeelezwa kuwa agizo hilo lililotolewa na Ofisa
elimu huyo linatekelezwa baada ya kuagizwa na Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri hiyo, Hussein Ngaga kwamba afanye hivyo na fedha ziingizwe kwenye
jina la akaunti hiyo jambo ambalo wamesema, kitendo hicho ni wizi wa fedha za
wananchi hivyo ni vyema zikafuatwa taratibu husika za kumpata mzabuni kwa
kufuata taratibu zenye uwazi na sio vinginevyo, hivyo kutozingatia hilo ni
kukosa utawala bora na kuleta migogoro isiyokuwa ya lazima katika jamii.
Mwandishi wa habari hizi amefanikiwa kupata barua
yenye kumbukumbu namba W/E/MB/10/VOL.111/66 ya Januari 15 mwaka huu, ambayo
inawaagiza waratibu na walimu wakuu wote shule za msingi wilayani Mbinga,
kukusanya michango hiyo ya wazazi kwa ajili ya kuendeshea mitihani hiyo na
kuiingiza kwenye akaunti namba 62101600263 benki ya NMB, ambayo
ni ya Rukwa Computer Training Centre.
Sehemu ya barua hiyo inaagiza kwamba itafanyika
mitihani sita ya wilaya kwa darasa la saba mwaka huu, mitihani minne fedha
zitatoka kwa wananchi na miwili itatoka kwenye akaunti ya Capitation Grant,
hivyo mwanafunzi mmoja kwa mtihani mmoja anapaswa kuchangia shilingi 1,500 kwa
masomo ya Hisabati, Kiswahili, Sayansi, Historia, Uraia, Jiografia na
Kiingereza.
Kadhalika kwa upande wa darasa la sita, watakuwa na
mitihani miwili ambapo nao wanapaswa kuchangia shilingi 1,500 kwa kila mitihani
hiyo, kwa muhula wa kwanza mmoja na muhula wa pili mmoja.
Pamoja na mambo mengine nimezungumza na wadau
mbalimbali wa elimu wilayani humo, walisema kuwa kitendo hicho hakipaswi
kuvumiliwa kwani awali mitihani ya wanafunzi mashuleni ilikuwa ikichapwa kwa
kumpata mchapaji ambaye amepatikana kupitia mchakato halali wa zabuni husika,
hivyo wanashangaa jambo hilo kufanyika kwa siri na kuwaagiza waratibu na walimu
wakuu hao, wakusanye michango hiyo na kuiingiza kwenye akaunti ya mtu ambaye
wao hawamfahamu.
Hata wajumbe wa kamati za shule nao walieleza kuwa,
michango hiyo inayokusanywa kutoka kwa kila mzazi ambaye ana mtoto anayesoma
kwenye shule husika, na kuingizwa kwenye akaunti hiyo ni utaratibu mbaya wenye
kuonesha maslahi binafsi ndani yake, ambapo hivi sasa unaleta gumzo na
malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Walifafanua mfumo wa uendeshaji mitihani hiyo hasa
wakati wa likizo ni mpango ambao hata wazazi wa wilaya hiyo, walijiwekea
mikakati yao wenyewe na kujenga makubaliano juu ya namna ya kuinua kiwango cha
taaluma, kupitia vikao vya Mabaraza ya kata (WDC) hivyo wanashangaa kuona agizo
hilo lilitolewa na fedha ziingizwe kwenye akaunti ya mzabuni ambaye hafahamiki.
“Hapa tunavyozungumza kuna baadhi ya waratibu na
walimu wakuu wenzetu ambao wamekwisha ingiza fedha kwenye akaunti ya Rukwa
Computer Training Center, ni jambo ambalo sasa madiwani na wenyeviti wa shule
za msingi wamekuwa wakija juu na kuhoji kwa nini mambo yanafanyika bila kufuata
taratibu”, ? walisema.
WAZAZI
NAO WATOA YA MOYONI
Pia nimezungumza na Wazazi kwa nyakati tofauti nao
walisema, wanamshangaa Mkurugenzi huyo kuanzisha taratibu za kwake bila
kushirikisha wadau husika kupitia vikao mbalimbali, ambapo walifafanua kuwa
awali makubaliano yao kupitia vikao vya WDC haikuwa hivyo huku baadhi yao
wakisema ni vyema mfumo wa watoto kufanya mitihani mwishoni mwa mwezi,
akaziacha taratibu za awali kama wazazi walivyokubaliana katika vikao vyao
ambapo asipofanya hivyo mbele wanaona giza kwa maendeleo ya watoto wao kielimu
wilayani Mbinga.
“Kiongozi mzuri ni yule ambaye anashirikisha wenzake
na sio kuamua mambo yeye binafsi, kwa jambo hili tunamtaka afuate taratibu
ambazo sisi wazazi kwa kushirikiana na walimu wetu mashuleni kupitia vikao
halali, tulikwisha kaa na kuweka mikakati madhubuti ya kufanikisha watoto wetu
wakue kielimu hivyo tunasema hatuhitaji kurudishwa nyuma na mtu yeyote ambaye
hana uchungu na maendeleo ya wanambinga”, walisema.
Waliongeza
kuwa Ngaga tokea amefika katika wilaya ya Mbinga, ni mtu wa kupenda kutengeneza
migogoro ya hapa na pale kila kukicha badala ya kufikiria kufanya maendeleo ya
wananchi, hivyo ni wakati sasa kwa serikali kumchukulia hatua za kinidhamu ili
iwe fundisho kwake, na watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Walieleza kuwa michango wanayochanga wazazi kwa
watoto wao ili wajisomee hata wakati wa likizo, sio mpango uliowekwa na
serikali bali ni makubaliano yao na walimu mashuleni ambapo kufikia hatua ya
kuingiza fedha hizo kwenye akaunti ya mtu ambaye hajulikani ni wizi, na
kuingilia matakwa yao ambayo wamejiwekea wao wenyewe hivyo wamemtaka aache
kufanya hivyo badala yake afuate taratibu na sio vinginevyo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya
Mbinga, Ngaga alipotafutwa ili aweze kuzungumzia madai hayo, hakuweza
kupatikana ofisini kwake na simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila
kupokelewa.
Hata hivyo mwandishi wetu, alipozungumza na kaimu Afisa elimu
msingi wa wilaya ya Mbinga, Mwamwile alithibitisha kutolewa kwa agizo hilo
kwenda kwa waratibu elimu kata na walimu wakuu shule za msingi wilayani humo,
akiwataka fedha hizo ziingizwe kwenye akaunti hiyo ili mitihani ya watoto
mashuleni iweze kuchapwa.
No comments:
Post a Comment