Na Amon Mtega,
Songea.
MKAZI mmoja ambaye anaishi mtaa wa Changalae
kata ya Mletele Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Hamis Milanzi (68)
anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo, kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi
mwenye umri wa miaka (13) anayesoma shule ya msingi Luhila seko iliyopo
mjini hapa.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Kaimu
kamanda wa polisi wa mkoa huo, Yahaya Athumani alisema tukio hilo lilitokea
majira ya jioni katika mtaa huo ambapo mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo, baada
ya kumtishia mtoto huyo kwamba akikataa kufanya naye mapenzi atamfanya kitu
kibaya huku akimrubuni kwa kumpatia shilingi 30,000.
Yahaya alisema kuwa mwanafunzi huyo, ambaye
jina lake linahifadhiwa anaishi kata ya Mletele ambapo alikwenda nyumbani kwa
mtuhumiwa huyo kumdaifedha za kuni ambazo alimkopesha na alipowasili huko,
aliambiwa na mtuhumiwa huyo aingie ndani ili apewe fedha hizo.
Alisema baada ya kuingia ndani, ghafla
mwanafunzi huyo alijikuta anakamatwa kinguvu na kuanza kubakwa huku akimtishia
kuwa kama atapiga kelele atauwawa na kwamba asimwambie mtu yeyote, kutokana na
tendo alilofanyiwa.
Mara baada ya mtuhumiwa kukamilisha kufanya
unyama huo, alimwambia mwanafunzi huyo aendelee kubakia hapo nyumbani kwake na
kwamba alimuahidi kumpa fedha kiasi cha shilingi 30,000.
Kwa mjibu wa kaimu kamanda huyo, alisema
wazazi wa mwanafunzi huyo waliendelea kumtafuta kwa muda wa siku nne mtoto wao,
ambapo walimkuta kwenye duka lililopo maeneo hayo akiwa ananunua mahitaji
tayari kwa kwenda kufanya maandalizi ya kupika chakula nyumbani kwa
mtuhumiwa huyo ambaye alimgeuza mwanafunzi huyo akiwa mwandani wake.
Pamoja na mambo mengine, baada ya wazazi hao
kumuona walimfuata taratibu ili wajue anaingia nyumba gani, ndipo waliona
akiingia kwa Hamis Milanzi na ndipo taratibu za kumkamata na kutoa taarifa
kwenye vyombo husika zilianza kuchukua mkondo wake ambapo mpaka sasa polisi
wanaendelea na uchunguzi juu ya tuhuma hizo na mara utakapokamilika
mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu kosa linalomkabili.
No comments:
Post a Comment