Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre Baptiste Mapunda,
GAZETI la mwananchi, ijumaa iliyopita, Machi 13 mwaka huu
lilikuwa limebeba ujumbe mzito kwa Watanzania wenzangu, katika kichwa cha
habari, “Maaskofu: Pigieni Katiba kura
ya hapana.”
Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Kikristo (CCT) Askofu Dokta Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu
katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarcicius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste
Tanzania (CPCT) Askofu Daniel Awet kwa sauti moja, wamewataka waumini wao
kujiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura, kuisoma vyema katiba
pendekezwa na hatimaye kuikataa “kata kata” kwa kuipigia kura ya hapana.
Mosi ni kulazimisha kura ya maoni ya katiba mpya, kufanyika
bila maandalizi ya kutosha yakiwamo
maridhiano ambayo yameligawa taifa katika vipande vipande.
Pili viongozi waandamizi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuupigia debe muswada wa Mahakama ya kadhi, wakati wanajua kwamba kufanya
hivyo ni kukiuka misingi ya taifa ambayo Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliunda
taifa lenye serikali isiyo na dini.
Tamko hili nyeti ambalo limesambaa katika makanisa mengi ya
kikristo iwapo litasomwa kwa waumini wote na kuhamasishwa na mapadre,
wachungaji, na wainjilisti basi unaweza ukawa ndiyo mwisho wa katiba pendekezwa
kupigiwa kura 30 April mwaka huu.
Viongozi wa Jukwaa hilo wanawajibu wa kushiriki kikamilifu
katika zoezi hili la kuandika katiba mpya, ambalo linawahusu waumini wao pia. Tunatambua,
katiba si suala la siasa bali ni la Watanzania wote.
Itakumbukwa kuwa CCM, ilitumia mabavu na pesa nyingi sana
katika kusimamia mijadala ya katiba mpya
wakati mwingine hata kwa mitutu ya bunduki, wakapitisha katiba pendekezwa kwa kutumia
vyombo vya dola na wakakabidhiana
kwa kutumia mabavu pia.
Hofu ya kukataliwa kwa katiba mpya, kumeifanya serikali ya Jakaya
Kikwete ivunje kabisa makubaliano na TCD, kwamba kura ya maoni ingesitishwa
hadi baada ya uchaguzi mwaka 2016.
Lakini kwa sababu tu ya hofu ya kuanguka madarakani kwa CCM,
wameamua kuendelea kulazimisha kura ya maoni kwa kutumia mabavu
na kuwaburuza wananchi. Hii naweza nikasema ni alama au ishara ya
kuanguka kwa serikali iliyopo madarakani.
Matokeo yake inafanya kila hila ili daftari hili la wapiga
kura, lisiboreshwe na waweze kuchota kura vizuri kiholela holela. Nionavyo mimi hofu kuu hapa
ni katiba hii kuja kukataliwa na umma, hivi
Rais Kikwete ameona heri aendelee
kuisukuma walau ikubalike na umma.
Lakini ukweli ni kwamba katiba hii imekataliwa na wananchi
wengi pia hata na Mungu kwa sababu “sauti ya wengi ni sauti ya Mungu”.
Sababu nyingine kubwa ya kukataliwa na wananchi, wakiwamo
Maaskofu ni katiba pendekezwa yenye kulenga kulinda maslahi ya watu wachache
ndani ya chama na serikali ya CCM.
Kuvuruga uchaguzi kwa
kutumia katiba mbaya na kanuni mbaya ndiyo mwanzo wa machafuko, vita na mauaji
kama yale yaliyotokea nchini Kenya mwaka
2007, Kibaki alipolazimisha ushindi na akaapishwa usiku usiku mbele ya watu
wachache tu.
Katiba mpya inabidi ilete amani na siyo machafuko. Ukisoma
alama za nyakati hayo ndiyo yanayokuja mbele yetu hivyo Watanzania tujiulize
tunataka nini?
Katika mkutano wa Maaskofu hao uliofanyika tarehe 10 Machi
mwaka huu walisema kwamba; “Katiba inayopendekezwa imeleta mgawanyiko mkubwa
katika taifa hili, kwani imepatikana kwa njia zisizo za kiadilifu na mchakato
wake umeendeshwa kwa hila na ubabe”.
Viongozi hao kama wadau wa demokrasia, amani, na ustawi wa taifa
letu wamewaomba waumini wao
kujiandikisha kwa wingi katika daftari
la wapiga kura na kwenda kupiga kura ya “hapana” kwa katiba pendekezwa.
Maaskofu wana wajibu
na haki ya kutoa mwelekeo kwa waumini wao ili wachague kitu kizuri na siyo
kibaya kitakachokuja kuwadhuru hapo baadaye. Kama viongozi wa dini na jamii
hawawezi kuacha kuitahadharisha jamii juu ya hatari iliyopo mbele yao hatuwezi
kulipeleka taifa hili katika misingi ya uatwala bora.
Kwa upande wa UKAWA
wanaonekana kama walipata maono
ya kusoma alama za nyakati wakasusia bunge la katiba, uamuzi wa kutoshiriki
uovu huo ulikuwa mzuri na leo wapo huru kwamba hawakushiriki dhambi hii, ya
mauaji ya demokrasia nchini Tanzania.
Ikiwa mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba pendekezwa
umekiuka sheria ya mabadiliko ya katiba maana yake ni kwamba katiba pendekezwa ni feki, haina
uhalali wowote wa kisiasa, umekosa maridhiano na wala haukubaliki kwa
wananchi wazalendo wa Tanzania.
Lakini tamko hili la
Maaskofu hao wa Jukwaa la Wakristo linasema wazi kabisa na kushangazwa na kitendo cha serikali
kuahidi kuwapatia Waislamu Mahakama ya Kadhi kinyume na katiba ya nchi yetu. Tamko linasema kwamba
“kwa hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa katiba inayopendekezwa.”
Nimeshangazwa na tamko la Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwamba
makundi ya dini mbalimbali yamekuabiliana juu ya uwepo wa mahakama ya kadhi.
Ninamwomba waziri Mkuu “aache kuwa
sehemu ya tatizo la katiba na imani za dini
bali awe jawabu lenye kuleta amani, umoja, upendo na mshikamano” kwa
Watanzania kama alivyofanya Baba wa Taifa.
Maaskofu hao wanaendelea kubainisha jinsi usalama wanchi na
raia ulivyozorota na kuanza kuzalisha vikundi vya kihuni na ujambazi kama
“Panya road, Mbwa mwitu nakadhalika. Kama wadau wakubwa wa amani nchini wana
haki ya kuongelea suala hili nyeti kwa sababu amani ikitoweka viongozi wa dini
wanakuwa wa kwanza kulaumiwa kama ilivyotokea nchini Rwanda.
Tamko la Maaskofu hao “Kataeni katiba” naliona la “kinabii na
la kimapinduzi” lililokuja muda mwafaka ambapo waumini wa Kikristo walikuwa
hawana mwelekeo juu ya suala la kura ya maoni ya katiba pendekezwa, na suala la Mahakama ya
kadhi, ndiyo maana naandika Maaskofu wa Jukwaa la Kikristo wachochea moto wa
kuikataa katiba pendekezwa.
Mungu ibariki Tanzania na watu wake.
Mwandishi wa
makala haya anapatikana kwa barua epepe; frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment