Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAPIGA kura wa Jimbo la Tunduru kaskazini
mkoani Ruvuma, wamechukua jukumu la kumpendekeza Omary Kalolo, kuwa mgombea
pekee kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo, kwa nafasi
ya ubunge katika uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka
huu.
Shirikisho la umoja wa vijana la CCM wilayani Tunduru katika
jimbo hilo, ndilo ambalo limempendekeza mgombea huyo, kwa madai kuwa wanaimani
naye katika utendaji wa kazi zake.
Aidha vijana hao wamemtaka Kalolo kutoa tamko ambalo litaunga
mkono juu ya maamuzi na msimamo uliotolewa na shirikisho hilo, wakidai kuwa
yeye ndiye chaguo la wengi.
Msimamo wa kumtaka Kalolo kugombea, umejitokeza kupitia
risala yao iliyosomwa na Ally Nyama kwenye sherehe za ushindi wa asilimia 75
katika matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni mjini
Tunduru.
Walisema wameamua kutoa msimamo huo mapema kutokana na kukosa
imani na wagombea wengine (majina tunayo) ambao wanataka kujitokeza kugombea
katika jimbo hilo huku wakiwa hawana maaadili ya kichama.
Katika kuhakikisha kuwa nia yao hiyo inafanikiwa, vijana hao
walimkabidhi mgeni rasmi katika sherehe hizo, ambaye Mwenyekiti wa CCM wilaya
ya Tunduru Hamis Kaesa kiasi cha shilingi 100,000 ili zikae huko, ambazo zitamwezesha
mteule wao kwenda kuchukua fomu ya kuwania ubunge huo wakati utakapowadia.
Taarifa hiyo iliyoonekana kuungwa mkono kwa zaidi ya asilimia
60 ya wananchi walioshiriki katika sherehe hizo, vikiwemo vikundi vya kwaya ambavyo
viliendelea kufafanua katika nyimbo zao kuwa, Kalolo anao uwezo mkubwa wa
kuwaongoza kutokana na uzowefu alioupata wakati akiwa katibu wa chama hicho
ngazi ya wilaya na mkoa.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wanachama na wakereketwa wa
Chama Cha Mapinduzi ambao walihudhuria sherehe hizo, Nyama aliendelea kufafanua
kuwa maamuzi hayo hayatafanywa kwa kukurupuka, bali wameyafanyia uchunguzi wa
kina na kujiridhisha kuwa wagombea wote wanaotajwa kuwania nafasi hiyo hawana
sifa zinazomfikia mteule huyo.
“Sisi wanajimbo la Kaskazini kupitia tamko letu hili kwa
dhati na tunakuomba utoe tamko litakalojibu leo ombi letu hili, ambalo
litatuhakikishia ushindi katika jimbo letu kwani wewe ni hitaji la wengi”,
alisisitiza Nyama.
Alisema maamuzi hayo yametokana na mtazamo wa vijana wengi
katika Jimbo hilo, kuamini kuwa vijana ndiyo nguvu kazi hivyo ni bora nafasi
hiyo wampatie kijana mwenzao.
No comments:
Post a Comment