Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre
Baptiste Mapunda,
HOFU ya kukataliwa kwa katiba
mpya kumeifanya serikali ya awamu ya nne ivunje kabisa makubaliana na
TCD, kwamba kura ya maoni ingesitishwa hadi
baada ya uchaguzi 2016.
Hadi sasa hatujui nani atakuwa madarakani ni mpinzani au mwanaCCM mwenzao, hivi wanaona afadhali
waendelee kulazimisha kura ya maoni kwa
mtindo ule ule wa kulazimisha. Watanzania tunaelekea pabaya hii ni alama ya chama hiki tawala kukata
tamaa na kuanguka.
Matokeo yake inafanya kila hila, ili daftari la kudumu la wapiga
kura lisiboreshwe na waweze kuchota kura kirahisi, na ushahidi ukosekane.
Swali langu hapa ni kwamba, mbona Mwenyekiti wa tume ya
uchaguzi alisema wafadhili walishatoa pesa ya kuboresha daftari la wapiga kura?
Pia alisema hakuna uchaguzi utaendeshwa kuanzia sasa, bila kuboresha daftari
hilo?
Najiuliza nini kimetokea hapo katikati? na hofu yao nyingine
ni katiba hii pendekezwa kuja kukataliwa na umma, hivi Rais na serikali yake ya
CCM wameona heri waendelee kuisukuma ili ikubalike na umma wa Tanzania kwa
kutumia haya mabavu.
Lakini ukweli ni
kwamba, katiba hii imekataliwa na wananchi wengi na ina maana imekataliwa pia na Mungu, kwa
sababu “sauti ya wengi ni sauti ya Mungu.” Ukiisoma katiba pendekezwa binafsi
nasema utagundua kuwa ni ya kulinda maslahi ya watu wachache, ndani ya chama na
serikali hii ya CCM.
Kuvuruga uchaguzi kwa kutumia katiba mbaya na kanuni mbaya,
ndiyo mwanzo wa kuleta machafuko, vita
na mauaji kama yale yaliyotokea nchini Kenya
katika uchaguzi wa mwaka 2007.
Kibaki alilazimisha ushindi na akaapishwa usiku usiku, mbele
ya watu wachache tu. Ukisoma alama za nyakati unagundua kwamba hayo ndiyo
yanayokuja mbele yetu je tukae kimya?
Natambua ili kuielimisha jamii tunaandika bila hofu, ili
wananchi mjue kwamba serikali yetu sasa imepuuzia
kufanya maandalizi mazuri, ili kuhakikisha uchaguzi huru na wenye haki.
Uchaguzi wa haki na huru ndiyo ukomavu wa demokrasia unaoweza
kuepusha machafuko, vurugu, malalamiko na mauaji hapa nchini kupitia siasa
chafu zenye fitina, majungu na ukandamizaji.
Sasa kwa watanzania ili kuepusha katiba pendekezwa ya chama hiki tawala, isilete maafa kuna
mambo sita ya kufanya wananchi, vyama vya upinzani, madhehebu ya dini,
wanaharakati, wasomi na wananchi wenye mapenzi mema.
Mosi ni kwamba wadau
wa demokrasia, utawala bora na amani ambao ni wanasiasa, viongozi wa dini,
wanaharakati na wananchi wadai kuboreshwa kwa daftari la kupigia kura, ili kuwapa
watu wengi fursa ya kutumia haki ya kikatiba kupiga kura hasa vijana.
Kama kweli serikali ya CCM, ina amini juu ya demokrasia na
inasema inakubalika basi, wasiwe na hofu kukataa kuboreshwa kwa daftari hilo.
Pili, wapinzani na wadau wa siasa lazima wailazimishe serikali hii kuunda tume huru ya uchaguzi, ili
kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki kwa kila chama.
Jambo la tatu ni kwamba, sheria za uchaguzi ziboreshwe ili
kujenga mazingira ya usawa katika ushindani kwa vyama vyote. Kila chama kifuate
sheria na kanuni bila kujali CCM ni
chama tawala au la.
Mgombea binafsi aruhusiwe kama ilivyoamriwa na mahakama ya
rufaa. Hii ni katika kupanua uwigo wa demokrasia ya kweli kama kweli tunajigamba
kudumisha demokrasia na utawala nchini
Tanzania.
Jambo la nne na la msingi vyombo vya dola kwa maana ya Polisi,
Jeshi la wananchi (WTZ), FFU na usalama wa taifa visiingilie mchakato wa
uchaguzi, hata pale wanaponusa kwamba CCM inashindwa waiache kwani hii ndiyo
demokrasia ya kweli.
Zisitumike nguvu kubwa, bila sababu ya maana na hilo litaepusha vurugu kwani mara nyingi wanaoanzisha fujo na vurugu, katika vituo vya uchaguzi ni polisi na vyombo
vingine vya dola kwa kisingizio cha kulinda amani.
Hoja ya tano, kila chama kisaini makubaliano kwamba, kutokana
na mazingira hayo ya uwazi, basi atakayeshindwa akubaliane na matokeo. Hii ndiyo demokrasia ya kweli inayoambatana na utawala bora.
Jambo la sita wananchi wote wenye mapenzi mema na nchi yao
wahamasishwe, kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na siku ya uchaguzi wakafurike
vituoni, kwenda kupiga kura kwa kuchagua viongozi bora na siyo bora viongozi,
kwa sababu tu umepewa rushwa ya uchaguzi.
Kuhusu kura ya maoni ya katiba mpya, kuna ushauri mwingi unaoendelea
kutolewa na wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati, watu binafsi kwamba ni vyema
kura hiyo ikahairishwa kwa maslahi mapana ya taifa lote.
Kuna wanaotoa hoja kwamba, kuna haraka gani katika kupata
katiba mpya, kwani hata ikipitishwa haitaweza kutumika katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu. Mheshimiwa Rais Kikwete ameanzisha mchakato, basi ni hatua kubwa na
ya kumpongeza ili Rais ajaye awe wa CCM au wa upinzani basi ataendeleza hilo.
Ukawa walisusia mchakato wa katiba mpya na hivi inasemekana
wasingependa kushiriki, katika kuipigia kura katiba mpya kwani sio tunda la mawazo
na maoni ya wananchi kupitia Tume ya Mzee Warioba, bali ni mapandikizi ya
mawazo ya wanaccm walioteka Bunge nzima la katiba kule Dodoma.
Wananchi wengi wanafikiri kwamba, ikiwa mchakato mzima wa
upatikanaji wa katiba pendekezwa umekiuka sheria ya mabadiliko ya katiba maana
yake, katiba pendekezwa ni “feki” yaani haina uhalali wowote wa kisiasa, sababu mojawapo ikiwamo ukosefu wa maridhiano hivi kushindwa kukubalika na wananchi.
Ee Mungu wape hekima na busara viongozi wa serikali ya chama
hiki tawala, ili waupeleke mchakato huu
katika njia ya amani kwa manufaa ya taifa nzima, na sio kundi la watu wachache.
Ee Mungu uwajalie Watanzania ujasiri wa kukataa kuburuzwa na
serikali yao kwa sababu Siasa zinapita, lakini Tanzania haitapita kamwe. Tukumbuke kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni
kipimo cha ukomavu wa demokrasia na utawala bora katika nchi yetu ya
Tanzania Je, mtihani huu tutafaulu au
tutafeli? Mungu utusaidie!
Mwandishi wa
makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment