Na Mwandishi wetu,
WAKATI tukielekea uchaguzi mkuu mwaka huu, huku joto la
uchaguzi likiendelea kupanda miongoni mwa vyama vya siasa na wagombea wake, huenda
wakaanza kuonesha dalili ya kuibuka na sera mbalimbali ambazo huenda zikapewa kipaumbele,
katika uchaguzi huo.
Tumeshaona baadhi yao wakisema; ajira kwa vijana huku wakibashiri
kwamba endapo chama au mgombea ambaye katika ilani yake hatahusisha ajira kwa
vijana, huenda akapewa nafasi finyu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huu, ni
wosia toka kwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job
Ndugai.
Wapo waliodai “vijana
ni bomu” kwa kutaka tu kutoa tahadhari endapo hatutakabiliana na kutatua tatizo
la ajira kwa vijana, miongoni mwao hasa kwa wale wanaomaliza vyuo vikuu,
sekondari na shule ya msingi huenda ipo siku itafika na kuweza kuingia katika
wimbi la machafuko kama yalivyotokea katika nchi nyingine kama vile Misri,
Algeria na kwingineko.
Vivyo hivyo, tumewasikia wengine wakisema uchaguzi mkuu 2015
uwe wa vijana ambapo katika kundi hili wao wanataka rais kijana ili aje atatue
kero au matatizo ya vijana, kwa sababu anayafahamu hivyo ni rahisi kwake
kuyatatua na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu huku wakipigia chapuo, katika ajira
kama nguvu kazi ya taifa hili.
Binafsi sina tatizo na kundi lolote lile, ambalo limeibuka na
hoja hii ya ajira kwa vijana bali nawapongeza kwa kuliona hili mapema, ili
liweze kupata nafasi miongoni mwa watanzania walijadili na kuona ni kwa namna
gani, wanaweza wakaliweka sawa ili ifikapo kipindi cha uchaguzi waweze kupima
mgombea kutokana na sera zake na mikakati aliyonayo, katika kukabiliana na
tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Hoja yangu hapa ni kwa namna gani tunaitafsiri ajira kwa
vijana kulingana na mazingira ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ni wakati sasa tukaupanua
mjadala kuliko kuuminya ili kuweza kujenga mawazo mbadala yatakayoweza
kukabiliana na mazingira yetu ya kiuchumi na kijamii, kwa kuangalia ni kwa namna
gani tunaweza kuichanganua sera ya ajira kwa vijana.
Pia kabla ya kuidadavua kiundani sera ya ajira kwa vijana ni
vyema tukaweka angalizo ni kwa namna gani, tunajenga mazingira yanayoweza
kukidhi mahitaji ya muda mrefu kwa watoto na wazee pale tunapoitafsiri mikakati
ya ajira kwa vijana, kama nguvu kazi ili sera kwa vijana iwe na tija zaidi kwa
uchumi wa nchi na mahitaji muhimu ya watoto na wazee kwa ujumla wao.
Sambamba na hilo pia ipo haja ya kuangalia kwa kina na
kujifunza ni kwa namna gani nchi za wenzetu zilizoendelea, zimeweza kukabiliana
na tatizo la ajira licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu wake wenye kisomo cha
hali ya juu, wakiwa na rasilimali chache huku sisi katika mazingira yetu tuna
rasilimali nyingi na kushindwa kuzitumia ipasavyo pale tunapokabiliana na
tatizo hili la ajira kwa vijana.
Pia tujifunze ni kwa namna gani, tunaweza tukageuka nyuma na
kutazama sera zetu na kuzibadili kimfumo, kwa mfano licha ya Iran kuwa na
msuguano mkubwa na mataifa makubwa wamekubali kukaa meza ya mazungumzo na
mataifa hayo, na kwamba hadi sasa dalili zimeanza kuonekana za kuondoa vikwazo
huku lengo la wananchi wa Iran ni kulinda uchumi wao na ajira kwa vijana na sio
tu mitambo ya nyukilia ambayo wanayo
tokea miaka mingi iliyopita.
Mifano ipo mingi kwa kuanzia China, USA na nchi nyinginezo
hivyo ni vyema sasa tukapata kujifunza bila woga, na kamwe tusijifunge kimawazo
kwa hoja dhaifu eti hizo ni nchi zilizoendelea kiuchumi, sio rahisi kuweza
kuitumia mikakati waliyoitumia na sisi tukafanikiwa.
Mosi suala la sera
lisiwianishwe kwa vigezo tunavyotaka kuvitumia mfano umri wa mgombea, kufanya
hivi tunaweza tukashindwa kuitafsiri vema sera ya ajira kwa vijana endapo
tutakubali kuegemea katika vigezo vinavyoweza vikaathiri uchanganuzi mpana
zaidi, bali vimwandae au iwe ni nguzo katika kumpata kiongozi atakaye tekeleza
ajenda ya ajira kwa vijana kwa ufasaha zaidi.
Pili ni kwa namna gani tunalinda ajira kwa vijana wazalendo,
nashauri ni vyema tukabainisha ni mikakati ipi tutaiendeleza na kuibua kwa
manufaa zaidi ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.
Mfano tunaona mamlaka zetu zinatoa vibali kwa kupunguza kodi
kwa malighafi zetu kusafirishwa nje ya nchi.
Tatu ni kwa namna gani tunawatambua waajiri wadogo wadogo
wanaoweza kutoa ajira kwa vijana, mfano kuanzia watano na kuendelea ili waweze
kujenga uwezo mkubwa zaidi wa kuwaajiri vijana wetu na kutoa tija zaidi, katika
ujira na ajira kwa vijana wengi zaidi je upo mkakati huo na kama upo tunausimamiaje
na kama haupo tunawaza nini?
Nne tunawangaliaje wale waliojiajiri hata kwa zile sekta
ambazo sio rasmi, ila zina mchango mkubwa katika jamii. Mfano waponda kokoto
(zege) wauzaji vyakula maeneo ya barabarani, wale wanaojiita wapiga debe maeneo
ya stendi na wengine wengi katika nyanja tofauti.
Tano tunakabilianaje na kazi au ajira zinazoathiri mazingira
mfano kilimo maeneo yenye vyanzo vya maji, uchomaji wa mkaa, ufugaji usio na
tija. Licha ya juhudi za kusambaza umeme hata maeneo ya vijijini, nishati kubwa
yakupikia imekuwa ni kuni na mkaa hivyo tujipe tafakari endapo tutaendelea
kuona kila shughuli ni ajira, tujue ipo siku ukame utatufukarisha je, akinamama
ambao ni walezi wa familia watayapata maji wapi ukizingatia kwamba uharibifu wa
mazingira, ni kukaribisha ukame ambao baadaye ni balaa kwa viumbe hai.
Sita tuangalie ni kwa namna gani, waajiriwa wanakumbana na
changamoto mbalimbali hasa mikataba yao katika ajira na sheria zinazolinda
ajira zao, mfano tumeshawahi kuona serikali ikitangaza mishahara ya ajira
katika sekta binafsi lakini hadi leo imekuwa ni vigumu kujua ni kwa namna gani,
maagizo hayo yanatekelezwa mfano ajira za wafanyakazi majumbani, mashambani na kadha
wa kadha.
Saba inatupasa tuangalie mifumo yetu ya uwekezaji kama
inakidhi matakwa na matarajio ya watanzania kwa kiasi gani?, ni kwa namna gani
rushwa na uwajibikaji finyu unaathiri mchakato mzima wa kulinda na kutetea
ajira kwa vijana wetu wa kitanzania?, endapo tumeshindwa kukabiliana na rushwa
ndogo ndogo na ufisadi ambao unaendelea je hatuoni suala la rushwa na ufisadi
linaathiri mchakato mzima wa ajira kwa vijana wetu.
Nane tuangalie tija ya ajira na ujira kwa mapana zaidi, ili
iweze kukidhi matakwa ya kiuchumi na kijamii na tufikirie zaidi kutokana na
mazingira yetu ni kwa namna gani huyu kijana wakati ana nguvu analiingizia
taifa faida, je ni ipi kinga yake afikiapo uzeeni?, ipi kinga ya huyu kijana
kwa familia yake mfano watoto wake pamoja na mambo mengi zaidi ya hapo, tusiishie
kuimba wimbo wa ajira tu.
Tisa tunawianishaje suala la ajira na sekta mbalimbali za
uzalishaji mali ni kwa namna gani, tunabuni miradi mikubwa na midogo ya muda
mfupi na muda mrefu ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana wetu kutokana
na historia ya siasa yetu, maana tulishawahi kuambiwa ajira millioni moja
lakini hadi leo tunaona vijana wetu wakijaa uwanja wa taifa kugombania nafasi
70, je ndio hizo tulizoahidiwa million?
Kwa maoni yangu binafsi tunapochambua sera na mikakati ya
ajira kwa vijana, ni lazima tuichambue kwa mapana zaidi na kuiwekea mikakati
kwa misingi ya sekta na idara tofauti tofauti, ili ajira ziweze kuongezeka kwa
vijana kujiajiri wenyewe na wengine kuajiriwa, iwe ndani ya nchi au nje ya
nchi.
Hitimisho langu ni kwamba tunapozungumzia ukosefu wa ajira
tujue hakuna kiwanda kinachozalisha ajira, bali sera za uchumi ndizo
zitakazozalisha ajira hivyo siasa isiyo na mipango na mikakati ya kiuchumi sio
mwafaka na tija katika kukuza uchumi na kuzalisha ajira, hivyo mgombea atakayesema
ataongeza ajira, lazima apambanue ni kitu gani atafanya sio ajira za hewani au
kama anatoka usingizini, aeleze pia mipango na mikakati ya kiuchumi itakayoibua
ajira na sio kuishia katika propaganda za kisiasa tu ambazo nimejifunza katika
maeneo mbalimbali utekelezaji wake unakuwa mgumu.
No comments:
Post a Comment