Na Julius Konala,
Mbinga.
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)mkoa wa Ruvuma,
limechangia kiasi cha shilingi milioni 2.5 kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya
shule ya msingi Kihuruku, iliyopo wilayani Mbinga mkoani humo, kutokana na
majengo hayo kuwa katika hali mbaya ya uchakavu.
Mchango huo ulitolewa hivi karibuni na Meneja wa shirika hilo
mkoani hapa, Dickson Hawanga baada ya kujionea mazingira magumu ya shule hiyo
ikiwemo ukosefu wa choo, jambo ambalo linasababisha watoto kujisaidia
vichakani.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi hundi hiyo, kwa mwalimu
mkuu wa shule hiyo, Edmund Hyera Meneja huyo alisema anataka kuona fedha hizo
zinatumika ipasavyo kwa kazi iliyokusudiwa na sio vinginevyo.
Hawanga ameyaomba mashirika mbalimbali ya serikali na
yasiyokuwa ya kiserikali, watu binafsi pamoja na wahisani toka nje na ndani ya
nchi kumuunga mkono katika kuichangia shule hiyo, kwa kuipatia fedha au vifaa
vya ujenzi ili ukarabati uweze kukamilika kwa wakati.
Awali akisoma taarifa fupi ya shule hiyo mbele ya Meneja huyo
wa NSSF, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Edmund Hyera alifafanua kuwa shule yake
inakabiliwa pia na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ya bomba.
Hyera alisema, kuwa tatizo hilo linasababisha hata mahudhurio ya wanafunzi hao hivi sasa yamekuwa hafifu darasani, kutokana na baadhi yao kushindwa kuhudhuria vipindi kikamilifu kutokana na kuugua homa za matumbo, kama vile taifodi.
Alizitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo kuwa
ni upungufu wa nyumba za walimu, kwa madai kwamba zilizopo hazina hadhi ya
kuishi walimu ni uchakavu, uchakavu wa vyumba vya madarasa pamoja na upungufu
wa walimu kwa kipindi kirefu sasa ambapo ina jumla ya walimu saba, kati ya hao
wanaofanya kazi ni watano huku mahitaji yakiwa walimu tisa.
Kadhalika wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi wa
shule hiyo walidai kwamba kukosekana kwa maji ya bomba kumewasababishia mara
kwa mara kuugua magonjwa hayo, ambapo kichocho na kuwashwa mwili kutokana na
kutumia maji machafu yasiyo salama kwa afya ya binadamu.
Kufuatia hali hiyo Mbunge wa Jimbo la Mbinga mashariki,
Gaudence Kayombo ameahidi kuchangia bati, nondo na mifuko ya saruji kwa ajili
ya kusaidia ujenzi wa vyoo bora vya walimu na wanafunzi wa shule hiyo, ambapo
awali Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kupitia afisa elimu vifaa na takwimu,
Pendo Ndumbaro imetoa viti na meza 14 kwenye shule hiyo vinavyotokana na
chenchi ya Rada, huku akiahidi kuwaongezea vingine kutokana na kujionea ukubwa
wa tatizo la shule ya msingi Kikhuruku.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Paschal
Ndunguru, alilishukuru na kulipongeza
shirika la NSSF kwa kuchangia shule hiyo na kuwataka wananchi kujenga
utamaduni wa kushirikiana na serikali, katika kuchangia shughuli
mbalimbali za maendeleo badala ya kuachia kila kitu kifanywe na Halmashauri.
No comments:
Post a Comment