Makada mbalimbali Chama Cha Mapinduzi wakiweka mashada katika kaburi la Kapteni Komba, mara baada ya mazishi kufanyika kijijini Lituhi wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma. |
Na Mwandishi wetu,
Nyasa.
WAKATI Rais Kikwete akiongoza
watanzania, katika mazishi ya Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, Kapteni John
Komba kijiji cha Lituhi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, Rais mstaafu wa Malawi
Dokta Bakili Mluzi ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na
wananchi wa jimbo hilo, kwa kumpoteza mbunge huyo ambaye ni kipenzi cha
watanzania na wanamalawi.
Katika salaam zake alizotuma kwa
njia ya barua pepe na kusomwa makaburini hapo mbele ya Rais Kikwete na
waombolezaji wengine, Dokta Mluzi alisema kuwa anatambua mchango mkubwa wa
marehemu Komba hasa enzi ya uhai wake.
"Nimepokea taarifa hii ya kifo
cha mbunge wetu Komba kwa masikitiko makubwa, nipo pamoja na familia na
wananchi wote wa jimbo la Mbinga Magharibi katika maombolezo haya", alisema.
Spika wa Bunge, Anne Makinda
alieleza kusikitishwa kwake na manabii wa uongo ambao wamekuwa wakiendelea
kueneza uongo katika Taifa hili, kwamba lengo lao kuona halitawaliki kwa
utulivu na amani.
Alisema kuwa baadhi ya manabii hao ambao
wamekuwa wakizunguka huku na kule kwa wananchi, kazi yao ni kupandikiza chuki
juu ya katiba mpya iliyopendekezwa kwa kudanganya umma kuwa ndani ya katiba hiyo,
kumeingizwa kipengele kinachoonyesha ndani ya katiba hiyo kuna jambo lenye kuona
waislamu wanafanya mambo yao manne, likiwemo la talaka, mirathi na mengine kama
ambavyo dini nyingine zinafanya.
"Jambo kubwa hapa linalosumbua ni
juu ya manabii wa uongo wengi wao wanavumisha tu jambo hili halina ukweli, nasema
kwa sababu nafsi yangu inanituma niseme hapa hivi sasa, linalosumbua ambalo
litakuja katika bunge na mswada tayari ninao ni uwazi wa kufanya mabadiliko ya
sheria ya kiislamu iliyopo katika vitabu vya kiislamu mwaka 1964",
alisema.
Mwaka 1964 wakoloni walifanya
marekebisho na kuwa mahakama za mwanzo ndizo zilianza kufanya shughuli hizo.
Alisema mswada huo si mpya kinachofanyika
ni kuona waislamu wanaendelea kufanya mambo yao yanayowahusu kama vile mirathi,
talaka, vifo na ndoa wafanye wenyewe na sheria hiyo ipo tayari na sio kwamba
inatungwa upya.
" Ila wataalam wa manabii wa
uongo wanaeneza kuwa mambo haya yapo katika katiba inayopendekezwa nawaomba
sana msiwasikilize...........na lilifanyiwa kazi karibu wiki tatu
usiku na mchana kuona suala hilo haliwepo lakini wapo watu wanaotangaza kuwa
lipo huo ni uongo mkubwa, CCM ilijadiliana na makundi yote na halipo katika
katiba inayopendekezwa", alisema.
Spika Makinda alitaka dini zote kuendelea
kufanya Kazi zake kwa uhuru, bila kusikiliza hao wanaofanya kazi ya kueneza
uongo huo, kwa kutaka kuona nchi haitawaliki kutokana na uongo wanaoeneza.
Katika mazishi hayo yaliyoshirikisha
mawaziri mbalimbali akiwemo Waziri mstaafu, Edward Lowassa ambaye aliambatana
na mbunge wa Korogwe vijijini Steven Ngonyani maarufu kwa jina la Profesa Maji
Marefu, alitumia msiba huo kujipambanua zaidi kuhusu urafiki wake na Lowassa
kuwa kamwe hataacha kumuunga mkono Lowassa, popote atakapokwenda.
Profesa maji marefu ambaye alisafiri
na ndege moja na Lowassa, alisema anajisikia faraja kuendelea kujenga urafiki
na rafiki yake huyo, kwani hata kama atagombea urais kamwe hatacheza mbali na Lowassa.
"Mimi na Lowassa ni marafiki wa
siku nyingi, hatujaanza leo urafiki wetu wa damu ni mengi amenisaidia hivyo
nipo pamoja na Lowassa, kama mnavyoniona leo tupo hapa kumzika rafiki yetu
Komba", alisema.
Kwa upande wake mwakilishi wa kambi
ya upinzani bungeni Lindi mjini, Salum Baruan (CUF) mbali ya kumlilia mbunge
Komba, bado alisema kuwa Komba alikuwa ni msaada mkubwa katika vita dhidi ya
mauwaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini, na siku zote bungeni alikuwa
mpambanaji wa watu wanaoua albino.
Mbali ya mbunge huyo pia wabunge
zaidi ya sita waliokuwa katika kamati ya maendeleo ya jamii, makamu mwenyekiti
wakiongozwa na mbunge Said Mtandi alisema kifo chake kimekuja wakati wakiwa
mbioni kwenda ziara ya kimafunzo nchini Ephiopia.
Wabunge wengine walioshiriki ni
pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye alisema kifo cha
Komba si tu ni pigo kwa wananchi wa Mbinga Magharibi pekee, bali hata katika
wilaya hiyo ambapo mara kadhaa wameungana katika kuwatoa hofu wananchi wa
mwambao wa ziwa Nyasa, juu ya kuwa na hofu ya vita kutokana na chokochoko za
mipaka kati ya Malawi na Tanzania.
Filikinjombe alisema, kwa umoja wao
walipata kusogeza maendeleo katika wilaya ya Nyasa na Ludewa na kuwa kifo chake
ni pengo kubwa.
Akitoa salamu za serikali Waziri wa
nchi ofisi ya waziri mkuu, sera na uratibu wa bunge, Jenista Mhagama alisema
serikali imempoteza mtu muhimu katika Taifa hili, ambaye alitumia kipaji chake
kutoa elimu kwa watu mbalimbali.
Huku Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Taifa, Abdulahman Kinana akieleza kuwa, Komba alikuwa ni hazina kubwa ya chama
hichona kwamba kifo chake ni pigo kwao.
Mawaziri wengine walioshiriki
mazishi hayo ni pamoja na Steven Wassira, Profesa Mark Mwandosya, Dokta Fenela
Mkangala, pia mbunge wa Chalinze Ridhiwan Kikwete na Ritta Kabati ambaye ni mbunge
wa viti maalum mkoa wa Iringa.
Wakati huo huo wananchi wa Jimbo
hilo la Mbinga Magharibi walishindwa kujizuia kutokwa na machozi wakati mwili
wa Komba ukishushwa kaburini.
Huku wananchi hao wakitokwa na
machozi, baadhi ya makada wa CCM wanaotaka ubunge katika jimbo hilo, na wale
wanaotaka urais wapambe wao walionekana kutumia msiba huo kupiga kampeni waziwazi
huku fulana za wagombea zikiwatibua nyongo, watu wa usalama na baadhi yao
kutolewa mbele ya waombolezaji wakiwataka kwenda kuvua fulana hizo za kampeni.
No comments:
Post a Comment