Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imewasha rasmi mitambo ya kurushia matangazo ya digitali mkoani Ruvuma,
ili kuendana na mfumo wa kisasa wa mabadiliko ya sayansi na teknolojia na
kuachana na mfumo wa analogia.
Tukio hilo
la uzinduzi limefanyika jana katika kituo cha televisheni ya taifa TBC
mjini songea, ambapo ndipo ilipo mitambo hiyo ya kurushia matangazo ya
dijitali na mgeni rasmi wakati wa ufunguzi huo alikuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma,
Thabit Mwambungu.
Katika tukio hilo Mkurugenzi huyo wa TCRA,
Habbi Guze amewaagiza watoa huduma za usambazaji wa ving’amuzi walioko
mjini songea, kuhakikisha wanakuwa na ving’amuzi vya kutosha ili kuwafanya
wananchi, waweze kupata matangazo na taarifa mbalimbali za habari kwa wakati.
Pia alisema, serikali inatarajia
kupata ushirikiano wa karibu wa kutoa huduma kwa wadau wa sekta ya
utangazaji na wananchi kwa ujumla, katika kuhakikisha kwamba wakazi wa mjini
songea na mkoa huo kwa ujumla, wanapata huduma mpya ya matangazo ya
televisheni kwa mfumo wa digitali bila bugudha ya aina yoyote ile.
Guze alisema pamoja na kufikia hatua ya
kutumia mitambo hiyo mipya, lakini kuna vyombo vingine havitaguswa na mfumo huo
kama utangazaji wa satelaiti waya (cable)na radio, hivyo wakazi wa Songea
wasitupe TV zao au luninga za analojia kwa kuwa chanel tano za
kitaifa zitakuwa zinaendelea kupatikana, ingawa siyo kwa viwango vya ubora kama
vya dijitali.
Alisema katika mikoa yote iliyozimwa mitambo
ya analojia na kuwashwa mitambo ya dijitali, Ruvuma peke yake ndiyo iliyopata
mitambo ya kisasa zaidi kwa kuwa imeboreshwa ikiwemo kuwepo kwa
ving’amuzi vidogo na vyenye uwezo mkubwa, wa kurusha matangazo.
Kwa upande wake, Said Mwambungu aliipongeza
mamlaka hiyo pamoja na makampuni ya usambazaji wa mitambo hiyo, kwa kufanikisha
kuweka matangazo ya mfumo wa kisasa ndani ya mkoa wa Ruvuma na kuufanya
ufunguke kimaendeleo zaidi.
Alisema japokuwa mkoa huo umechelewa sana
kupata mitambo ya digitali, lakini bado wananchi wamelipokea kwa nguvu kubwa
kwani wengi wao walishaanza kutumia teknologia hiyo, hata kabla ya uzinduzi huu
kufanyika mjini hapa juu ya matumizi mapya ya mitambo hiyo.
No comments:
Post a Comment