Na Julius Konala,
Songea.
KAMPUNI ya Majembe Auction Mart Limited, inakusudia
kuifikisha Mahakamani Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa kile
kilichoelezwa kuwa imevunja mkataba wa ukusanyaji ushuru (Service Levy) kinyume
na utaratibu, jambo ambalo limeisababishia kampuni hiyo, hasara zaidi ya
shilingi milioni 70.
Mkurugenzi wa kanda katika kampuni hiyo, Nelson Mwasomola alisema
hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, juu ya kitendo
cha uvunjwaji wa mkataba huo ambao umefanywa na Halmashauri hiyo.
Mwasomola alisema kusimamishwa kwa kampuni yake, kutoendelea
na kazi ya ukusanyaji wa ushuru huo kumesababisha kushindwa kufikia malengo ya
ukusanyaji wa fedha kwa kiwango husika kilichowekwa kwa kila mwezi, na
kusababisha kuwepo kwa hasasra kubwa.
Aidha Majembe Auction Mart, ni kampuni ambayo iliomba kazi ya
ukusanyaji wa ushuru wa huduma (Service Levy) na kwa bahati nzuri ilishinda
tenda lakini cha kushangaza wamesimamishwa kuendelea na shughuli hiyo, bila
sababu za msingi na kuisababishia hasara kubwa, kutokana na gharama ya kuwekeza
jambo ambalo limeifanya kushindwa kumudu kuwalipa mishahara wafanyakazi
wake, pamoja na kodi ya nyumba.
Kadhalika alieleza kuwa pamoja na kampuni hiyo kusimamishwa
kuendelea na kazi hiyo, cha kushangaza halmashauri ya Manispaa ya Songea
imekuwa ikiendelea kukusanya fedha kwa kutumia kibali cha kampuni ya Majembe
Auction Mart kinyume na utaratibu, ambapo mpaka sasa halmashauri imefanikiwa
kukusanya kiasi cha shilingi milioni 25 kupitia vielelezo mbalimbali walivyokuwa
wakivitumia kukusanyia ushuru kampuni hiyo.
Alieleza kwamba, imekuwa ni mazoea kila kampuni inapoomba
kazi na kushinda zabuni hunyang’anywa tenda bila ya kujali gharama za uwekezaji
na uendesdhaji jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara, na kwamba mbali ya
kuandika barua mbalimbali za kutaka ufafanuzi juu ya jambo hilo, mpaka sasa
hawajajibiwa chochote.
Kampuni imekusudia kwenda Mahakamani, huku halmashauri hiyo ikiwa
imepewa hati ya mashtaka (notisi) ya siku 30 ya kusudio la kufikishwa kwenye
chombo hicho cha sheria, na kutolea maelezo kwa maandishi sababu
zilizopelekea kuvunjwa kwa mkataba huo.
Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri
ya Manispaa ya Songea, Nachoa Zakaria alipohojiwa na gazeti hili kuhusiana na
tuhuma hizo alidai kwamba hazina ukweli wowote ndani yake, na ofisi yake
haijatoa barua yoyote kwa kampuni hiyo juu ya kuvunjwa kwa mkataba wa kukusanya
ushuru huo.
No comments:
Post a Comment