Kapteni Komba akiwa Bungeni Dodoma enzi ya uhai wake, akichangia mada mbalimbali. |
Kassian Nyandindi na Mashirika mbalimbali ya habari,
MBUNGE wa Mbinga Magharibi, Kapten John Komba ambaye alifariki
dunia jana jioni Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye amesikitishwa kutokea kwa kifo hicho.
Mmoja wa watoto wa Komba ambaye aliyejitambulisha kwa jina la
Herman alikuwa akizungumza huku analia, kwamba msiba wa baba yake upo nyumbani
kwake Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam.
Habari zinasema asubuhi ya Februari 28 mwaka huu, Komba
alikwenda kwenye shughuli zake za kikazi kama kawaida lakini baadaye akajisikia
vibaya, hivyo akaamua kurudi nyumbani ambako alizidiwa ndipo familia yake
ilipoamua kumkimbiza Hospitali ya TMJ, lakini alipopimwa na madaktari
ikathibitika kuwa alikuwa tayari ameaga dunia.
Kapteni Komba ambaye pia ni Mkurugugenzi wa kikundi cha maigizo,
Tanzania One Theatre (TOT) ambacho kina kikundi cha taarabu na bendi
inayokwenda na mtindo wa Achimenengule, amekuwa akikisaidia sana chama chake,
Chama Cha Mapinduzi katika kampeni zake wakati wa uchaguzi kwa kutunga nyimbo
za kuhamasisha wapiga kura na kushiriki kupiga live, kwenye majukwaa ya
kisiasa.
Alipokuwa Bungeni:
Enzi ya uhai wake alitamani sana na kufanya juhudi
kubwa ili mtindo wa Achimenengule uwe wa kitaifa lakini ikashindikana, na
badala yake Watanzania sasa tuna muziki wa mduara ambao umekuwa kama mtindo wa
muziki wetu, kwa sababu zifuatazo.
Kwanza, ni mtindo halisi wa kitanzania uliochipuka kutoka
mahadhi ya kimwambao ya Tanzania.
Pili, ndiyo mtindo pekee uliowahi kutumiwa na bendi nyingi baada
ya kuasisiwa na mabingwa wa muziki wetu, wana njenje, the Kilimanjaro band.
Baada ya bendi hiyo kuiasisi kwa mtindo huo, tayari umepigwa
na bendi kama TOT Plus, Chuchu Sound, Pamo Sound, Inafrika Band, wana mipasho
kadhaa na mwanamuziki mahiri lakini asiyethamini kiwango chake kikubwa cha
muziki, Bob Haisa.
Sababu ya tatu ni kwamba mtindo huo umekuwa wa kupigwa na
bendi nyingi, vikundi vingi na wanamuziki wengi si kwa kulazimisha, bali kwa
mapenzi tu ya mashabiki wa muziki wa Tanzania.
Kapteni Komba awali alikuwa mwalimu wa shule ya msingi kabla
ya kuingia Jeshini na kuwa kiongozi wa kikundi cha maonesho cha jeshi na
baadaye Rais mstaafu Alli Hassan Mwinyi akamshawishi aachane na jeshi na
kujiunga na CCM, wakati wa mfumo wa vyama vingi ulipoanza hapa nchini mwaka 1992.
“Mzee Mwinyi ndiye aliyenifanya niache jeshi wakati huo
nikiwa na cheo cha ukapteni. Aliniomba nikisaidie chama kwa kuanzisha kikundi
ambacho lengo lake lilikuwa kukipigia debe CCM,” aliwahi kusema hivyo Kapteni Komba
enzi ya uhai wake.
Pia ameshiriki kampeni za marais Ally Hassan Mwinyi, Benjamin
William Mkapa na aliye madarakani hivi sasa, Jakaya Mrisho Kikwete. Alikuwa
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi
hadi kifo kinamchukua.
Licha ya siasa Kapteni Komba alikuwa anamiliki shule na pia
alikuwa na biashara kadhaa. Mwaka 2012 Komba aliwahi kupelekwa India kwa
matibabu ambapo alifanyiwa upasuaji wa nyonga, baada ya kupata ugonjwa
uliosababisha mifupa kusagana sehemu hiyo ya nyonga.
Baada ya kurejea nchini alisema upasuaji huo ulichukua saa
tano na ulifanyika katika Hospitali ya Apollo, India na alikanusha kuwa alikuwa
na ugonjwa wa figo na kurejea hapa nchini Julai 27 mwaka 2012. Ugonjwa uliomuua
ni shinikizo la damu ambalo lilikuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
Marehemu ameacha mjane, Bi Salome, ambaye ni mwalimu
kitaaluma na watoto kadhaa.
No comments:
Post a Comment