Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
LAURENT Kibasa (30) ambaye ni dereva wa pikipiki, mkazi wa
mtaa wa Kiwandani Mbinga mjini mkoani Ruvuma, amepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya wilaya hiyo, kwa tuhuma ya kumlawiti mwanaume mwenzake (Jina
tunalo) mwenye umri wa miaka 24 na kumdhuru mwili.
Mwendesha mashtaka msaidizi wa polisi, Inspekta Seif Kilugwe
alidai mbele ya Hakimu Joachimu Mwakyolo wa Mahakama ya wilaya ya Mbinga, kuwa mshtakiwa
huyo alitenda kosa hilo Aprili 23 mwaka huu majira ya mchana akiwa nyumbani
kwake baada kushindwa kulipwa deni analodai shilingi 85,000.
Kibasa anadaiwa kufanya makosa hayo kwa dereva wa pikipiki
mwenzake maarufu kwa jina la Boda boda, baada ya kumfuata kwenye eneo lake la
kazi kisha kumkamata na kumpeleka
nyumbani kwake ambako anadaiwa alimfunga kamba mikononi na kuanza kumpiga, kwa
kutumia mkanda wake wa suruali.
Inspekta Seif alieleza Mahakamani hapo kuwa, mshtakiwa huyo
wakati anafanya hilo pia alikuwa akimpiga kwa mateke na ngumi na baadaye
alimbeba na kumpeleka chooni, ambako alimvua suruali aliyokuwa ameivaa na
kumfanyia kitendo hicho cha kinyama.
Pamoja na mambo mengine, Kibasa amekwisha somewa maelezo hayo
ya awali na alikana shitaka hilo linalomkabili na kwamba limepangwa kusikilizwa
tena, Mei 5 mwaka huu na mshatakiwa yupo nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment