Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
JUMUIYA ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, umeazimia kumuenzi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la
Mbinga Magharibi, Marehemu Kapteni John Komba kila mwaka ifikiapo Februari 28
wataandaa matamasha mbalimbali ikiwemo kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.
Aidha siku hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya kuwakusanya,
wananyasa waishio nje ya Nyasa, kurejea kwao na kusaidia kuchangia ukuaji wa
uchumi wa wilaya hiyo na maendeleo ya wananchi kwa ujumla ili waweze kuondokana
na umasikini.
Kwa kutambua umuhimu na mchango mkubwa wa maendeleo
uliofanywa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Kamanda wa jumuiya hiyo ya umoja
wa vijana wilayani Nyasa, Cassian Njowoka alisema hayo alipokuwa katika ziara
yake ya kikazi wilayani humo wakati alipokuwa akizungumza kwenye baraza la
vijana kata ya Kilosa.
Njowoka alisema, marehemu Komba muda wake mwingi enzi ya uhai
wake alikuwa akipigania kwa nguvu zake zote maendeleo ya wananchi wake, wakiwemo
vijana ambapo muda mwingi alikuwa akiwahamasisha wajiunge pamoja na kuanzisha
vikundi vya ujasiriamali.
“Sisi kama vijana lazima tujitoe kwa nguvu zetu zote
kumuenzi, ametufanyia mambo mengi ambayo
tukiyazingatia yatatusaidia kuepukana na umasikini, nawaombeni wazo hili
liungwe mkono na wananyasa wote”, alisema Njowoka.
Alisema mwaka huu unatarajiwa kufanyika uchaguzi mkuu, hivyo
vijana wanapaswa kuwa makini kwa kutokubali kutumiwa na wale ambao wamekuwa na
tamaa ya madaraka, ambapo jukumu lao kubwa ni kuwachuja ili kuona kama kweli
watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia, pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya
kuwaongoza.
Njowoka alisema jumuiya ya vijana ni tegemeo kubwa katika
kufanikisha ushindi wa chama, hasa nyakati za chaguzi hivyo kinachotakiwa ni
kuhakikisha wanakuwa na mshikamano wa dhati na kwamba, wasaidie kutangaza kwa wananchi
yale yote yaliyotekelezwa kwa vitendo kama ilivyoainishwa ndani ya ilani ya
uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
Alisema vyama vya upinzani, siku zote vimekuwa na kawaida ya
kuwatumia vijana kwa kuwadanganya wakiuke sheria za nchi ikiwemo kuandamana bila
kibali halali, huku wao wenyewe wakirudi nyuma, jambo ambalo mwisho wake husababisha
vijana hao kukumbana na matatizo makubwa ikiwemo hata kupelekwa mahakamani.
Kamanda huyo wa vijana wa wilaya ya Nyasa, alisema wakati
umefika sasa kwa vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi, lakini pia wahamasishe wale ambao sio wanachama wa CCM wajiunge ili
kuongeza idadi ya wanachama.
No comments:
Post a Comment