Wednesday, April 8, 2015

MTOTO APOTEZA MAISHA BAADA YA KUTAFUNWA NA WANYAMA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MTOTO wa mfugaji mwenye asili ya Kisukuma, walioweka makazi katika kijiji cha Twendembele kata ya Ligunga wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, aliyefahamika kwa jina la Shija Luchoma (15) amefariki dunia na mwili wake kuliwa na wanyama wakali, baada ya kuvamiwa wakati akichunga ng’ombe porini katika kijiji hicho.

Taarifa za tukio hilo, zinafafanua kuwa marehemu huyo alikumbwa na mkasa huo baada ya kushambuliwa na mnyama ambaye bado hajafahamika, wakati akiwa machungani kwenye hifadhi ya Selou kijijini humo.   

Baba mzazi wa kijana huyo, Masanja Luchoma alisema tukio lilitokea Machi 26 mwaka huu ambapo marehemu alikuwa ameondoka nyumbani kwake na kundi la ng’ombe hao kwa ajili ya kwenda kuwachunga waweze kupata malisho, ambapo baadaye ilimshangaza mnamo majira ya jioni aliona ng’ombe wakiwa wanarudi peke yao.


Kufuatia hali hiyo, mzazi wa mtoto huyo kwa kushirikiana na majirani wenzake walipochukua jukumu la kufanya ufuatiliaji ndipo walikuta mabaki ya mwili wa marehemu yakiwa katika msituni kwenye hifadhi hiyo.

Aidha Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi amethibitisha juu ya hilo na kuongeza kuwa uchunguzi unafanyika ili kuweza kubaini kama kweli mtoto huyo alipoteza maisha kwa kuliwa na mnyama, na taarifa kamili kutolewa baadaye.


Pamoja na mambo mengine, Dokta Vitaris Lusasi alifafanua kuwa mtoto huyo ameshambuliwa na mnyama mkali, huku akivitaja baadhi ya viungo ambavyo alivifanyia uchunguzi na kuthibitisha hilo kuwa ni fuvu la kichwa, vidole, kiganja cha mkono na kipande cha mguu wa kushoto.

No comments: