Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
IMEELEZWA kuwa ushirikiano uliopo kati ya wananchi wa vijiji
vya Lunyere kilichopo wilayani Nyasa nchini Tanzania na Mpapa wilaya ya
Lagunyasa jimbo la Lichinga Msumbiji, umetakiwa kudumishwa ili amani na utulivu
uliopo mpakani kati ya nchi hizo mbili uweze kuendelea.
Hayo yalisemwa na Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka alipokuwa akizungumza
na wananchi mara baada ya kumwapisha kamanda wa jumuiya hiyo kata ya Mpepo
Bosco Kihwili, sherehe ambayo ilifanyika katika kijiji cha Lunyere.
Njowoka alisema wananchi wa Lunyere, hususani vijana wamekuwa
wakijihusisha na shughuli za uchimbaji madini ambapo kutokana na uhusiano mzuri uliopo kwa muda mrefu baina ya nchi
hizo mbili, wengi wao wamekuwa wakivuka mpaka na kwenda Msumbiji ambako pia
hufanya shughuli za uchimbaji bila kikwazo hivyo ni vyema wakazingatia sheria
zilizopo ambazo zinapaswa kufuatwa pindi wanapotaka kuingia nchi hiyo jirani.
Alisema kuwa ameelezwa kwa muda mrefu viongozi wa vijiji
hivyo, wamekuwa wakitembeleana na kusaidiana katika shughuli za kimaendeleo na
kwamba hata imefika wakati kujenga undugu kati ya wananchi wa vijiji hivyo.
“Nimefurahi sana leo, kuona viongozi wa kijiji jirani cha
Msumbiji kualikwa katika sherehe hizi hii inaonesha wazi uhusiano ambao umedumu
kwa muda mrefu kati yenu unaendelezwa, kama ulivyoasisiwa na viongozi waasisi
wa nchi hizi”, alisema Njowoka.
Akizungumza katika sherehe hizo mara baada ya kupewa nafasi,
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mpapa nchini Msumbiji, Alexandria Mundau
Kosa alisema dhamira ya chama chao cha FRELIMO ni kuendelea kudumisha
ushirikiano huo baina ya nchi hizo na kwamba aliwapongeza viongozi wa juu wa
pande hizo mbili, kwa kuendeleza mahusiano hayo ambayo yalikuwepo kabla hata ya
nchi hizo kupata uhuru.
Mundau Kosa alipongeza jitihada zinazoendelezwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na serikali yake kwa kufungua mipaka, ikiwemo ujenzi wa
barabara ambao unaziunganisha kitendo ambacho imeelezwa kuwa, kitasaidia
wananchi wa pande hizo kunufaika kwa namna moja au nyingine.
Kadhalika Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lunyere,
Anderson Haulle alisema wataendelea kudumisha ushirikiano huo ili wananchi wake
waishi kwa amani na utulivu na kwamba hawatakuwa na suluhu, kwa wale ambao
watajitokeza kuleta vurugu au uvunjifu wa amani ambayo mwisho wake itasababisha
kuzorotesha mahusiano mazuri yaliyopo kati yao.
No comments:
Post a Comment