Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akikabidhi Mwenge wa uhuru kwa Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani humo, Profesa
Norman Sigalla kwa ajili ya kuanza mbio zake katika wilaya ya Songea.
|
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta
Alli Mohamed Shein amekemea kitendo kinachofanywa na baadhi ya watu kuwagawa
Watanzania, jambo ambalo linahatarisha amani ya nchi yetu.
Dokta Shein alisema kumekuwa na makundi ambayo huwagawa kwa
misingi ya dini, rangi na ukabila jambo ambalo amekemea vikali na kutaka hali
hiyo iachwe mara moja.
Vilevile alikemea vitendo vya biashara ya madawa ya kulevya, ambapo alieleza kuwa kundi la vijana ndilo kwa kiasi kikubwa linahusika na
vitendo hivyo na kuwataka waachane na tabia hiyo badala yake wafanye shughuli
za kimaendeleo, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Rais huyo alifafanua kuwa ni aibu kwa taifa hili vijana
kujihusisha na biashara hiyo, kwani wao ndio nguvu kazi katika kusukuma
gurudumu la maendeleo hivyo serikali itaendelea kupambana na vitendo hivyo vya
uuzaji wa madawa hayo, ili visiweze kuendelea.
Alisema yote hayo yanatokana na kundi hilo la vijana, kuwa na tamaa
ya kutaka kupata utajiri kwa uharaka na njia zisizo halali.
“Ninawaomba Watanzania wenzangu kila mmoja wetu pale alipo
akae na kutafakari, kwa kukemea kwa nguvu zote juu ya biashara hii ya madawa ya
kulevya hasa kuwafichua wale wanaofanya ili tuweze kuondokana na hali ya
kuliabisha taifa letu”, alisema.
Pia Shein amewataka wakimbiza Mwenge, kutoa ujumbe kwa
wananchi ipasavyo kwani wao taifa limewaamini katika kutekeleza jukumu hilo
muhimu.
Kwa upande wake, Waziri wa habari, utamaduni na michezo,
Dokta Fenera Mkangara alisema mbio hizo za Mwenge ni tunu ya taifa na zimekuwa
zikisaidia kuelimisha jamii kwa makundi yote, na kuitaka janmii kutumia haki
yao ya kidemokrasia katika kupiga kura kwenye katiba ijayo na uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu mara baada ya
kukabidhiwa Mwenge huo alisema utakimbizwa katika mkoa huo kuanzia Aprili 29
hadi Mei 4 mwaka huu, ambapo ukiwa mkoani humo utaweza kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 41 yenye
thamani ya shilingi bilioni 10.3 katika wilaya tano za mkoa huo.
Hata hivyo ameitaja miradi itakayokaguliwa, kuwekewa mawe ya
msingi na kuzinduliwa kuwa ni ya sekta ya maji, afya, maliasili, miundombinu,
elimu na kilimo ambapo Mwenge huo wa uhuru ameanza kukimbizwa mkoani Ruvuma
katika Halmashauri ya Songea na baadaye kuelekea wilaya ya Mbinga.
No comments:
Post a Comment