Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
WATOTO wanaosoma katika shule ya msingi Nangombo wilayani
Nyasa mkoa wa Ruvuma, wapo hatarini kuangukiwa na majengo ya shule hiyo
kutokana na kuwa chakavu na kutofanyiwa ukarabati kwa zaidi ya miaka 80.
Akizungumza na wazazi wa shule hiyo, Kamanda wa umoja wa
vijana (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka alielezwa na mkuu wa shule hiyo,
Hyasint Hyera kuwa majengo hayo ni machakavu na yapo hatarini kuanguka kufuatia
kuwepo kwa nyufa sehemu mbalimbali.
Hyera alisema kuwa shule ilianzishwa mwaka 1932 na kwamba
inawanafunzi 290 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, lakini pamoja na
kutolewa taarifa mara kwa mara kwa viongozi wa serikali hakuna hatua
zilizochukuliwa jambo ambalo ni hatari kwa watoto hao.
Alifafanua kuwa changamoto mojawapo inayowakabili shuleni
hapo, ni kukosekana kwa vitendea kazi ikiwemo chaki za kuandikia pale mwalimu
anapokuwa darasani akifundisha wanafunzi, hali ambayo ilisababisha watoto hao
kukaa katika kipindi cha wiki tatu bila kufundishwa.
Mwanafunzi Desderia Ndunguru wa darasa la saba alisema, mara
nyingi kutokana na mazingira ya shule hiyo kuwa magumu, wakati mwingine
wanapokuwa darasani wamekuwa wakiingiliwa na wadudu wa aina mbalimbali wakiwemo
nyoka, nge na kenge na kuwafanya baadhi ya watoto washindwe kuhudhuria masomo
ipasavyo kutokana na kuogopa wadudu hao.
Desderia aliwaomba viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa
kutembelea shuleni na kutatua changamoto zilizopo, ili wanafunzi wapate
mazingira mazuri ya kusomea ambayo yatapelekea kufanya vizuri kwenye masomo
yao.
Kwa upande wake akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa UVCCM
wilayani humo Njowoka alisikitishwa na mazingira mabovu ya shule ya msingi
Nangombo jambo ambalo alisema ni udhalilishaji wa watoto ambao ni taifa la
kesho na kwamba aliwataka wazazi, viongozi na watendaji wa wilaya hiyo kujenga
tabia ya kutembelea shule zote zilizomo wilayani humo, ili kubaini changamoto
mbalimbali zinazowakabili walimu na wanafunzi.
Njowoka aliwaasa wananchi wa Nyasa ambao wanaishi nje ya
wilaya, kusaidia jitihada za maendeleo zinazofanywa na wananchi ili kuimarisha
ustawi wa maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Aidha kufuatia changamoto zinazoikabili shule hiyo, Kamanda
huyo wa umoja wa vijana aliweza kutoa msaada wa chaki, kalamu za wino vifaa vya
michezo na kutoa ahadi ya kununua mashine ya kutengeneza chaki, ili kupunguza
tatizo la uhaba wa chaki katika shule za wilaya hiyo.
Hata hivyo kutokana na uchakavu wa majengo ya shule hiyo
ambayo inatakiwa kujengwa upya, ili kuweza kuwanusuru wanafunzi kukumbwa na
maafa ya kuangukiwa na majengo hayo Kamanda huyo wa vijana, ameahidi
kushirikiana na wazazi kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa ambapo yeye
atagharimia vifaa vyote vya viwandani.
No comments:
Post a Comment