Gari la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambalo lilisababisha mauaji, baada ya kumgonga dereva wa pikipiki na mtembea kwa miguu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
DEREVA aliyekuwa akiendesha gari la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, Emmanuel Millanzi
amenusurika kuuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya gari alilokuwa
akiliendesha, kugonga na kuua watu watatu papo hapo.
Gari hilo ambalo ni aina ya Everest, lenye namba za usajili AAA
217 MN nalo limenusurika kuteketezwa kwa moto na wananchi hao ambao walishikwa
na hasira kutokana na ajali hiyo, kwa kile kilichodaiwa kusababishwa na dereva
huyo ambaye alikuwa akiliendesha kwa mwendo kasi.
Waandishi wa habari ambao waliwasili katika eneo la tukio, walielezwa
na mashuhuda wa ajali hiyo kuwa gari hilo lilikosa mwelekeo kutokana na kuwa katika
mwendo huo, hatimaye kwenda kumgonga mwendesha pikipiki na abiria wake na
mtembea kwa miguu ambao wote walipoteza maisha.
Kaimu kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malinyi
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilitokea Aprili Mosi mwaka
huu, majira ya saa 3:15 asubuhi katika eneo la mtaa wa Ruhuwiko darajani Mbinga
mjini.
Malinyi alisema kuwa Millanzi wakati anaendesha gari hilo,
lilimshinda wakati alipotaka kukata kona ambayo ipo katika eneo la daraja hilo
hatimaye gari kusababisha mauaji hayo na kwamba baada ya kuona wananchi wana
hasira na kutaka kumjeruhi, alijisalimisha kwa kukimbia ambapo hivi sasa naye
amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga kutokana na kuwa na maumivu
katika mwili wake.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Benadetha Mapunda (18) mtembea
kwa miguu mkazi wa mtaa wa Ruhuwiko, Lusekelo Mwaisimba (32) mwendesha pikipiki
mkazi wa mtaa National Housing na abiria wake Teddy Ndunguru (25) ambaye pia ni
mhasibu wa kanisa la TAG Mbinga mjini.
Wakati huo huo Machi 31 mwaka huu, majira ya mchana katika eneo la
pacha nne Manispaa ya Songea mkoani hapa, gari aina ya Hino bus lenye namba za
usajili T 927 BGZ lililokuwa likiendeshwa na dereva, Said Mwale (35) liligonga
pikipiki yenye namba za usajili T 446 CCS aina ya SUNLG iliyokuwa ikiendeshwa
na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Fredy ambapo baada ya kugongwa,
pikipiki hiyo nayo iligonga gari jingine lenye namba za usajili T 119 AFD aina
ya Toyota Pickup lililokuwa likiendeshwa na Kelvin Francis (55).
Baada ya tukio hilo, dereva wa pikipiki Fredy na abiria aliyekuwa
amembeba Philomena Kiwele (26) wote wawili walipoteza maisha papo hapo huku
dereva wa gari, Mwale alitokomea kusikojulikana baada ya ajali hiyo kutokea.
Katika tukio jingine, alfajiri Aprili Mosi mwaka huu majira ya saa
10:20 katika eneo la Lilambo barabara ya Songea, Mbinga watu wanne walipoteza
maisha kutokana na gari lenye namba za usajili T 499 ADB Toyota Carina
lililokuwa linaendeshwa na Kanuth Millanzi (28) kugongana uso kwa uso na gari
lenye namba za usajili T 788 DUP aina ya Senya ambaye dereva wake hafahamiki,
alitelekeza gari hilo na kukimbia kusikojulikana.
Vilevile katika ajali hiyo, mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Fatuma
Jafary ambaye alikuwa amekodi gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Millanzi
kwenda Hospitali ya Misheni Peramiho kwa ajili ya matibabu, ambapo alikuwa na
watoto wake wawili mapacha na binti yake wa kazi hivyo baada ya ajali hiyo
dereva huyo, watoto hao mapacha na binti huyo wa kazi walipoteza maisha papo
hapo huku mama huyo akiwa mahututi na kukimbizwa hospitali ya mkoa Songea,
ambako amelazwa na mpaka sasa hali yake ni mbaya.
Hata hivyo, wakati huu kuelekea sikukuu ya Pasaka Kaimu kamanda wa
Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Malinyi amewaasa madereva na watembea kwa miguu
kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali ambazo zimekuwa
zikitokea mara kwa mara huku takwimu zikionyesha katika mkoa huo, ajali nyingi
husababishwa na uzembe wa madereva au wakati mwingine watembea kwa miguu.
No comments:
Post a Comment