Na Steven
Augustino,
Tunduru.
WAKULIMA katika kata ya Muhuwesi, wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma wamewataka watendaji katika vijiji vya wilaya hiyo, kujenga ushirikiano wa
karibu ili kuweza kusukuma mbele maendeleo yao.
Rai hiyo ilitolewa na wakulima wa Chama cha ushirika cha
Mumsasichema AMCOS, walipokuwa kwenye kikao chao cha wadau wa zao la korosho
kilichofanyika katika ofisi za chama hicho kijiji cha Muhuwesi wilayani humo.
Mwenyekiti wa chama hicho, Issa Kambutu alifafanua kuwa
kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko mkubwa wa maadili ikiwemo kukithiri kwa
vitendo vya wizi wa fedha za wakulima wa zao hilo, ukifanywa na baadhi ya viongozi
hao sasa kuna kila sababu kujenga ushirikiano ili kuweza kudhibiti hali hiyo.
Kambutu alisema vitendo hivyo vya wizi vinafanyika hasa
kipindi cha msimu wa zao hilo, ambacho ushuru hukusanywa na kwamba aliwataka
kuwa na uzalendo ambao utaifanya hata Halmashauri ya Tunduru kuwa na mapato
makubwa.
Watendaji hao wa vijiji, wanadaiwa kushirikiana na wanunuzi
binafsi kufanya biashara ya kununua korosho kwa kuingia uwakala na makampuni
binafsi ambayo ndiyo husuka mipango ya kupoteza mapato ya halmashauri na
kuwanyonya wakulima wa zao hilo.
Awali akisoma taarifa ya mapato ya ununuzi wa korosho katika
msimu wa mwaka wa 2013/2015 mwandishi mkuu wa AMCOS hiyo, Said Akimu aliwaeleza
Wajumbe wa mkutano huo kuwa chama chao kilifanya manunuzi ya kilo 378,648 zenye
thamani ya shilingi milioni 454,377,600 kiasi ambacho alidai kuwa ni kidogo
hakilingani na hali halisi ya uzalishaji unaofanywa na wakulima wa wilaya hiyo.
Hali hiyo imeelezwa kuwa imetokana na viongozi husika
kutotimiza wajibu wao ipasavyo, ikiwemo kusimamia mapato ya chama kuhakikisha
kwamba hayachakachuliwi ili kuweza kufikia malengo.
No comments:
Post a Comment