Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
KITENDO cha akina mama wajawazito kulala na kujifungulia
chini ya sakafu katika Zahanati ya kijiji cha Lunyere, kata ya Mpepo wilayani
Nyasa mkoa wa Ruvuma, kimemshangaza Kamanda wa Jumuiya Umoja wa Vijana ya Chama
Cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka na kuwataka wadau mbalimbali
kujitokeza kuchangia vifaa mbalimbali vinavyokosekana, hali ambayo itasaidia akina
mama hao na wananchi kwa ujumla wapate huduma za afya katika mazingira salama.
Kushangazwa huko kulitokea baada ya kutembelea katika eneo
hilo na kutoa msaada wa vitanda 20, magodoro 20, mito ya kulalia, mashuka na
vyandarua vifaa ambavyo tokea ijengwe haikuwa navyo jambo ambalo lilisababisha
wagonjwa wengi kupata huduma duni wanapokwenda kupata matibabu.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho wakati akikabidhi
vifaa hivyo, Njowoka alisema ameguswa na kero hiyo inayowakumba wananchi hao
ambapo analazimika kuendelea kutoa mingine ikiwemo mabomba ya maji, umeme wa
nguvu ya jua na kukamilisha ukarabati wa chumba cha kujifungulia akina mama hao
wajawazito.
Njowoka aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Lunyere, kwa
kuchangishana shilingi milioni 40 ambazo zimetumika kufanikisha ujenzi wa
zahanati hiyo huku akiutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa, kuunga
mkono juhudi zilizofanywa na wananchi wa kijiji hicho ambacho kipo upande wa
kusini mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
“Ningependa kuona kambi ya vijana wa kata hii ya Mpepo
wanaiweka hapa Lunyere, lakini kazi kubwa iwe kujishughulisha jambo ambalo
litakuwa msaada katika kukamilisha ujenzi wa zahanati hii, ikiwemo kufyatua
tofari zitakazosaidia ujenzi wa nyumba za kuishi waganga”, alisema Njowoka.
Awali kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho,
Anderson Haulle alisema mpaka kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo hakuna
mchango wowote uliotolewa na serikali, jambo ambalo linawasikitisha wananchi na
kujiona kama wametengwa na viongozi wao waliowachagua na watendaji wa
Halmashauri hiyo, ambao wamepewa dhamana
ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Haulle alisema Lunyere ni kijiji ambacho wanaishi wachimbaji
wa madini ambapo moja ya kero waliyokuwa wakikabiliana nayo kabla ujenzi wa
zahanati hiyo, ni kutokea kwa vifo vingi na maiti zilikuwa zinahifadhiwa katika
ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho kitendo ambacho kimsingi ni udhalilishaji wa
binadamu.
Naye Mganga mkuu wa zahanati hiyo, William Ndimbo alifafanua
kuwa magonjwa yaliyoshamiri kijijini hapo ni malaria, kuharisha, kichomi,
magonjwa ya zinaa na Ukimwi na kwamba changamoto kubwa inayowakabili ni
upatikanaji wa madawa ambapo kutokana na kituo kutosajiliwa na Bohari ya madawa
ya binadamu (MSD) hulazimika kupata madawa kutoka wilayani.
Hata hivyo Ndimbo alimshukuru Kamanda huyo wa Jumuiya ya
umoja wa vijana kutokana na moyo wake wa kutoa vifaa hivyo, na kwamba ahadi
yake ya kutoa madawa yenye thamani ya shilingi milioni moja kila mwaka
itasaidia kutoa kero ya upatikanaji wa madawa, huku akiwataka wadau wengine nao
wajitokeze kusaidia ili waweze kuondokana na matatizo mbalimbali
wanayokabiliana nayo katika sekta hiyo ya afya.
No comments:
Post a Comment