Saturday, April 4, 2015

MKURUGENZI MBINGA AHUSISHWA NA KASHFA YA UVUNAJI MSITU BILA KUSHIRIKISHA WANANCHI

Rais Jakaya Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WENYEVITI wa vitongoji vya kata ya Matarawe wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu baada ya wananchi wa kata hiyo kuwajia juu na kuwataka wajiuzuru katika nafasi zao za uongozi, kutokana na suala la uchanaji mbao katika msitu wao bila kuwashirikisha.

Aidha wananchi hao, wamemnyoshea kidole Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga kwa kile walichoeleza kuwa ndiye anayevuna msitu huo ambao unafahamika kwa jina la Mbambi, bila kutoa taarifa kwao.

Hayo yalijitokeza Aprili 2 mwaka huu, katika mkutano walioketi kwenye uwanja wa shule ya msingi Kipika mjini hapa, ambapo wananchi hao walionekana kujawa jazba huku wengine wakizomea na kutotaka kuelewa juu ya hoja iliyoletwa mbele yao na Afisa mtendaji wa kata ya Mbinga mjini, George Maliyatabu.

Kwa mujibu wa maelezo ya afisa mtendaji huyo alisema kuwa yeye alikuwa ametumwa na Mkurugenzi huyo mtendaji, awaeleze wananchi kwamba anawaomba samahani juu ya jambo hilo hivyo atafanya nao kikao cha pamoja ili aweze kuzungumza juu ya tukio hilo, kitendo ambacho kiliendelea kuamsha hasira na kumtaka aondoke katika mkutano huo yeye pamoja na wenyeviti wa vitongoji ambao alifuatana nao.


Wenyeviti hao wa vitongoji waliokataliwa mbele ya mkutano huo ni Philibert Hyera wa kitongoji cha Kipika, David Ndimbo kitongoji cha Lulambo, Gisberth Ndimbo wa kitongoji cha Pugulu na Said Makunganya kutoka kitongoji cha Matarawe.

Kadhalika wakichangia hoja katika mkutano huo, Wolta Komba ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Matarawe alisema wenyeviti hao ndio wanaoshiriki na Mkurugenzi Ngaga kuvuna msitu wao kinyemela, bila kushirikisha wananchi ambapo wanamashaka nao hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kuwaongoza badala yake waachie ngazi.

“Hawa viongozi wetu hawatufai mpaka miti hii inavunwa walikuwa wapi, hawa ni wanafiki mmetekwa na mkurugenzi na kufikia hatua ya kupoteza mali za wananchi, kwa manufaa yenu binafsi”, alisema Komba.

Naye Denice Hyera mkazi wa kitongoji cha Kipika alifafanua kuwa, mbao katika msitu huo wa Mbambi zimekuwa zikivunwa nyakati za usiku na mchana huku magari ya Halmashauri, yakionekana kubeba na kupeleka kusikojulikana.

Hyera alieleza kuwa kitendo hicho kinawafanya wapoteze imani na viongozi wa ngazi ya juu ya wilaya hiyo, huku wakihusisha jambo hilo ni sawa na wizi kutokana na wananchi kutopewa taarifa juu ya upasuaji wa mbao katika msitu huo.

Alisema kwamba msitu huo ni tegemeo kubwa ambapo upo kwenye chanzo cha maji, hivyo kukatwa kwa miti na kuendelea na shughuli ya upasuaji mbao kunahatarisha kutoweka kwa uoto wa asili na maji kupotea.

“Tumechoka kila kiongozi anayefika hapa Mbinga kazi yake ni kuvuna misitu yetu bila wananchi kunufaika, shule zetu za msingi na sekondari kuna uhaba mkubwa wa madawati ya kukalia wanafunzi, kwa nini usingewekwa mpango mzuri wa kupasua mbao na kutatua tatizo hili na sio kujinufaisha mtu mmoja”?, alihoji Hyera.

Pamoja na mambo mengine, mwandishi wa habari hizi ameshuhudia mbao 454 ambazo zimekamatwa na wananchi hao zikiwa zimekusanywa na kuwekwa pamoja katika chumba kimoja cha shule ya msingi Kipika, huku pia wakizuia shughuli za upasuaji zisiendelee kufanyika ndani ya msitu huo ambazo zilikuwa zikifanywa na Felix Mbilinyi ambaye alipohojiwa alisema ametumwa na uongozi wa wilaya hiyo.


Hata hivyo alipotafutwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo ya wananchi hakuweza kupatikana na hata alipopigiwa simu ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

No comments: