Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
KATIKA kuhakikisha kwamba zao la korosho linaboreshwa na kuwa
endelevu, halmashauri wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imetenga zaidi ya
shilingi milioni 10 kwa ajili ya kufufua na kuendeleza zao hilo katika maeneo
mbalimbali wilayani humo.
Kati ya fedha hizo shilingi milioni 5 zitatumika kununua
miche ya zao hilo na shilingi milioni 5 zinazobakia zitatumika kwa ajili ya
kununua mbegu za korosho kutoka chuo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele kilichopo
mkoani Mtwara.
Zao la korosho. |
Afisa kilimo umwagiliaji na ushirika wilayani Namtumbo,
Ally Lugendo aliyataja maeneo yatakayonufaika na mpango huo ni pamoja na kata
ya Magazini, Lusewa, Msisima, Ligera, Lisimonji, Limamu, Likuyu, Mchomoro na
Rwinga ambapo mbegu na miche hiyo itasambazwa katika maeneo hayo ambayo yana
hali nzuri ya hewa inayostawi vizuri korosho.
Alisema kuwa halmashauri imefikia uamuzi wa kufufua zao la korosho
baada ya kuwepo kwa soko la uhakika katika kipindi cha msimu wa mwaka huu
ambapo bei imepanda kutoka shilingi 1,500 kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,000
jambo ambalo halmashauri inaamini kwamba kama wakulima wataamua kuwekeza katika
kilimo hicho wataweza kuondokana na umaskini katika familia zao.
Lugendo alisema kufufuliwa kwa zao la korosho na hata mazao
mengine ambayo yalisahaulika kwa muda mrefu ni mkakati wa
halmashauri kuhakikisha wakulima wanakuwa na mazao mengi ya
biashara ambayo halmashuari inayaona kama vyanzo mbadala
ya vya mapato hasa ikizingatia kuwa asilimia 90 ya wakazi wake
wanategemea kilimo kama njia kuu ya uchumi.
Katika msimu wa mwaka 2015/2016 halmashauri ilianza pia
na mpango wa kulima zao la kahawa na kununua miche 16,668 ambayo tayari imesambazwa
kwa wakulima msimu wa mwaka huu na miche 33,330 imeongeza kutoka chuo cha
utafiti wa zao la kahawa TaCRI Ugano, kilichopo wilayani Mbinga mkoani
humo.
Lugendo alizitaja kata zenye hali nzuri ya hewa inayofaa kwa
kilimo cha kahawa ni pamoja na kata ya Likuyu, Litola, Mgombasi, Namabengo,
Msindo na Namtumbo ambazo hali yake ya hewa ni baridi tofauti na ilivyo kwa maeneo
mengine.
Afisa ardhi na maliasili wa wilaya ya Namtumbo, Mauruce Hyera
alisema kuwa, halmashauri imetenga imetenga kilometa za mraba 1,000 ambazo
zitatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji
na makazi.
Hyera aliongeza kuwa bado wilaya hiyo ina eneo la kilometa za
mraba 5,791 hazijatumika na kwamba zinahitaji wawekezaji mbalimbali wa ndani na
nje ya nchi kwenda kuwekeza kwa ajili ya shughuli za kilimo.
“Sisi kama halmashauri tayari kuna maeneo tumeyatenga kwa
ajili ya shughuli za kilimo, idara ya ardhi ipo tayari kutoa kila aina ya
ushirikiano kulingana na mwekezaji husika atahitaji kuzalisha zao gani”,
alisema.
No comments:
Post a Comment