Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema
kwamba katika tuhuma ambazo zimefikishwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, juu ya suala la utoroshaji wa zao la kahawa ni lazima
shauri hilo lifikishwe Mahakamani ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo
wake.
Cosmas Nshenye. |
Nshenye alisema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake kufuatia kukamatwa kwa mfanyabiashara, Khatwib Rajabu
mkazi wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera akidaiwa kushirikiana na wenzake kufanya
tukio la utoroshwaji wa kahawa wilayani hapa, bila kufuata taratibu na sheria
husika zilizowekwa na serikali.
“Hapa kesi lazima iwepo na kama sio kwa mfanyabiashara
aliyehusika kutorosha kahawa basi itabaki kwa watumishi wa serikali waliohusika
kutoa kibali hiki, huku wakijiua kwamba wanafanya makosa”, alisisitiza Nshenye.
Kwa ujumla taarifa za uhakika zilizomfikia mwandishi wetu kupitia
vyanzo mbalimbali vya habari zinathibitisha kuwa gari lenye namba za usajili T
533 BLR na T 188 BGH mali ya mfanyabiashara mmoja maarufu mjini, Godfrey Malila
ndilo lililohusika kwa namna moja au nyingine katika kutorosha kahawa hiyo
yenye kudaiwa kuwa ni zaidi ya tani 50.
Wataalamu kutoka idara ya kilimo halmashauri ya mji wa
Mbinga, ndio wanaonyoshewa kidole wakituhumiwa kuhusika juu ya utoroshaji huo ambapo
mnamo Novemba 9 mwaka huu majira ya mchana, waliokuwa wakitorosha kahawa hiyo
walikamatwa katika geti la mazao lililopo kijiji cha Kitai kata ya Mkako
wilayani Mbinga.
Awali Mkuu wa wilaya hiyo, Nshenye katika vikao vyake mbalimbali
vya kikazi amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kwamba, mtumishi
yeyote ndani ya wilaya hiyo asiyetaka kubadilika kwa kuongeza uwajibikaji mzuri
mahali pake pa kazi ni vyema akatafuta kazi nyingine ya kufanya au kwenda
wilaya nyingine, lakini sio kubaki Mbinga ambayo imekuwa na historia nzuri
ya wananchi wake kupenda kujituma kufanya kazi za kujiletea maendeleo bila kusukumwa.
Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akisema hayo kwa kupiga marufuku
juu ya utoroshwaji wa zao la kahawa ambao umekuwa ukifanywa mara kwa mara kwa
njia za ujanja wilayani humo na kuifanya wilaya hiyo kukosa mapato yake.
Hata hivyo jeshi la Polisi mkoani hapa, limethibitisha kukamatwa
kwa shehena hiyo ya kahawa na gari lililobeba zao hilo ambapo imeelezwa kuwa
watuhumiwa waliohusika kufanya hivyo wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani, ili
waweze kujibu tuhuma zinazowakabili mbele yao.
No comments:
Post a Comment