Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma
kwa tuhuma ya kuwashushia kipigo kikali watu wawili sehemu mbalimbali za miili
yao, wakituhumiwa kuiba kwenye nyumba ya kulala wageni ya Jordan River iliyopo
mtaa wa Majengo, Manispaa ya Songea mkoani hapa na kumsababishia kifo Anold
James mkazi wa Njombe mjini mkoani Njombe.
Zubery Mwombeji. |
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisini kwake,
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo
lilitokea Novemba 2 mwaka huu majira ya saa 12:40 asubuhi kwenye maeneo ya
nyumba hiyo ya kulala wageni mjini humo.
Mwombeji alifafanua kuwa inadaiwa siku moja kabla ya tukio
hilo kutokea watu wawili Anold James (25), James Exavery (18) wote wakazi wa Njombe
walifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni na kuomba chumba cha kulala na kwamba
kwenye kitabu cha wageni aliandikishwa mtu mmoja tu ambaye ni, Anold James
kisha baadaye James Exavery aliondoka akabaki Anold.
Alisema kuwa baadaye ilipofika majira ya saa za usiku kwenye
chumba hicho alichokuwa amelala Anold, kulisikika sauti kuwa kuna watu wengi
ndipo Meneja wa nyumba hiyo ya wageni Barnaba Said (22) alilazimika kwenda
kuwachungulia ambapo aliona wamekaa kwenye chumba hicho, huku wakinywa pombe na
baada ya muda mchache aligundua kuwa kunamali imeibiwa.
Said alieleza kuwa baada ya kugundua pia kaunta yake ya bar iliyopo
katika eneo hilo imeibiwa alimtaarifu mhudumu wa nyumba ya kulala wageni kuwa, hata
kwenye bar pia watu wasiofahamika wamevunja kaunta na kuiba na akamweleza kuwa
kwenye chumba alichopanga Anold anahisi kuwa kunawatu ndipo
walipoanza kumtaka Anold afungue mlango wa chumba chake, ambapo baadaye
kelele zilianza kusikika kwa majirani na umati mkubwa wa watu ulifika kwenye
eneo hilo huku ukimtaka Anold afungue chumba hicho.
Kamanda Mwombeji alieleza kuwa Anold alipofungua tu mlango
wa chumba chake ghafla kundi la watu wenye hasira kali waliwavamia watu
waliokuwemo kwenye chumba hicho na kuanza kuwashambulia kwa kuwapiga sehemu
mbalimbali ya miili yao, wakiwatuhumu kuwa ni wezi ambao wameiba kwenye nyumba
hiyo ya kulala wageni.
Vilevile katika tukio hilo kundi kubwa la watu walikuwa
wameizunguka nyumba hiyo ya kulala wageni huku baadhi ya watu wakilazimika
kutoa taarifa kituo kikuu cha Polisi Songea mjini, ambapo askari Polisi walipowasili
kwenye eneo la tukio waliukuta umati huo mkubwa wa watu ambao walipoona Polisi
walianza kukimbia na kutokomea kusikojulikana na kuwakuta watu wawili waliokuwa
wameshushiwa kipigo wakiwa mahututi.
Kamanda huyo aliongeza kuwa hatua ya kwanza waliwachukua
majeruhi hao na kuwakimbiza katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma, ambako baada ya
muda mfupi Anold James alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu na James
Exavery amelazwa na hali yake ni mbaya.
Pamoja na mambo mengine kufuatia kutokea kwa tukio hilo
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, ametoa mwito kwa wananchi kutochukua sheria
mkononi pale wanapowakamata watuhumiwa wa uhalifu na badala yake wanapaswa
wawafikishe kwenye vyombo vya sheria ili hatua husika za kisheria ziweze
kutekelezwa.
No comments:
Post a Comment