Na Muhidin Amri,
Tunduru.
WILAYA ya Tunduru mkoani Ruvuma, imeanza Operesheni maalum
ya kukabiliana na upungufu wa majengo ya umma ambapo hivi sasa ufyatuaji wa
tofari 100,000 kwa kila kijiji unafanyika, ili kuweza kupata matofari ya kujengea
majengo ya shule kama vile madarasa, nyumba za walimu, zahanati na vyoo.
Akiwa katika hafla ya kukabidhi matofari 7,642,816 kwa Mkuu
wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge katika vijiji vya Ligoma na Makoteni,
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera alisema kuwa, baada ya kubaini
wilaya yake ina upungufu mkubwa wa majengo hayo ya umma wameamua kuanzisha
operesheni hiyo ili kuweza kufikia malengo husika.
Homera alimweleza Dkt. Mahenge kuwa matofari hayo ni ya awali
tu na kwamba katika baadhi ya vijiji wananchi wanaendelea na kazi hiyo, ambapo
vijiji vingine wilayani hapa vipo katika hatua ya kuchoma tofari hizo na kwamba
zoezi hilo litakapokamilika wanatarajia kuwa na tofari 16,700,000.
Alibainisha kuwa hadi sasa tarafa ya Mlingoti imekabidhi
matofali 1,901,842 tarafa ya Matemanga 690,000 Namasakata 1,204600 Nalasi
1,365974 Lukumbule 955,000 Nakapanya 830,000 na Nampungu tofari 695,400.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge
alipongeza jitihada hizo zinazofanywa na wananchi wa wilaya ya Tunduru na
kuongeza kuwa waendelee kujitokeza kuchangia nguvu zao katika shughuli za
maendeleo, ili kuweza kukuza uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment