Damian Kapinga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Ruanda mara baada ya kukabidhiwa baiskeli maalum ya kutembelea. |
Mbinga.
CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa
Ruvuma, kimetoa msaada wa baiskeli maalum ya kutembelea mlemavu Damian Kapinga
(22) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili, shule ya sekondari Ruanda
wilayani humo yenye thamani ya shilingi milioni moja.
Akikabidhi msaada huo shuleni hapo mbele ya Mkuu wa shule
Stephano Ndomba na Diwani wa viti maalum tarafa ya Namswea Immaculatha Mapunda,
Mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa Martin Mbawala alisema kuwa baiskeli
hiyo ya kutembelea mtoto huyo imepatikana kutokana na jitihada zilizofanywa na
chama, kutoka kwa wasamaria wema.
Mbawala alisema kuwa chama kimefanya jitihada ya kutafuta
baiskeli hiyo kutokana na taabu alizokuwa akizipata mtoto huyo kutambaa kwa
mikono na magoti wakati wa kwenda shule kuhudhuria masomo yake, hivyo kiliona
kuna kila sababu ya kumtafutia chombo hicho ili kumrahisishia asiendelee kupata
adha hiyo.
“Nakukabidhi baiskeli hii iweze kukusaidia na kukurahisishia
uweze kutembea na kuhudhuria masomo yako vizuri, nawaomba viongozi wa kata hii
ya Ruanda muendelee kumtunza mtoto huyu kama walivyo wenzake ambao hawana
matatizo ya ulemavu”, alisisitiza Mbawala.
Kwa upande wake mwanafunzi Damian alitoa shukrani kwa CHAWATA
tawi la Mbinga, kumpatia msaada huo ambapo alisema ni mkombozi mkubwa kwake
kwani awali alikuwa akipata shida namna ya kutembea hasa nyakati za masika pale
mvua zinaponyesha.
Damian alieleza kuwa wakati huo wa mvua hasa pale
zinaponyesha, wanafunzi wenzake walikuwa wakilazimika kumbeba na kumpeleka
darasani ili aweze kuhudhuria masomo yake.
Vilevile Diwani wa viti maalum, Mapunda akizungumza kwa niaba
ya viongozi wenzake waliokuwa wamewasili wakati wa kupokea kiti hicho cha
kutembelea mwanafunzi huyo alitoa shukrani kwa Chama hicho cha walemavu tawi la
Mbinga kuona umuhimu wa kumsaidia mtoto huyo, huku akiongeza kuwa msaada kama
huo uendelee kutolewa kwa walemavu wengine pale panapojitokeza fursa ya
upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kusaidia watu wenye ulemavu.
No comments:
Post a Comment