Sunday, November 20, 2016

WAJASIRIAMALI SONGEA WANUFAIKA NA MIKOPO WASISITIZWA KUITUMIA KWA MALENGO YALIYOKUSUDIWA

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

WAJASIRIAMALI waliopo katika vikundi vya wanawake na vijana halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamepewa shilingi milioni 20 na halmashauri hiyo ili waweze kuendeleza vikundi vyao kwa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.

Fedha hizo walizopewa ni mkopo ambao unalenga kusaidia vikundi 42 vya wajasiariamali hao na sehemu ya mkopo huo watapaswa kurejesha baada ya miezi 12 ambapo kila kikundi kimepewa kuanzia shilingi 800,000 huku vingine vikipewa shilingi 600,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Ofisa habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo alisema kwamba vikundi vilivyopewa fedha hizo vimetoka katika kata 21 zilizopo katika Manispaa ya Songea.


Midelo alisema kuwa hii ni mara ya pili kwa halmashauri hiyo kutumia asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kutoa fedha hizo kwa vikundi vya vijana na wanawake, ambapo katika mwezi Julai mwaka huu waliweza kutoa mkopo wa shilingi milioni 52 kwa vikundi 107 ili waweze kuendeleza miradi yao.

Kadhalika kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji akizungumza wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya wajasirimali hao kabla ya kupewa mkopo huo, aliwaasa wanavikundi hao kutumia vizuri fedha hizo katika masuala husika na sio vinginevyo ili siku ya mwisho waweze kurejesha mikopo hiyo.

“Sisi Manispaa tunatoa riba ya asilimia kumi tu kwa mkopo wa mwaka mmoja, asasi nyingi za kifedha zinatoa riba kubwa yenye makato mengi hali inayosababisha wakopaji kushindwa kufikia malengo yao, hivyo nawaomba mkatumie vizuri mikopo hii”, alisisitiza.

Mshaweji aliongeza pia kwa kuwataka kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha hizo na wahakikishe wanarejesha kwa wakati ili ziweze kusaidia vikundi vingine vya wajasirimali katika Manispaa hiyo.

Nasisitiza zingatieni taratibu zote za mafunzo haya ambayo mmepewa, fedha hizi zisifanye mambo mengine ambayo hayapo katika mipango ya miradi yenu kumbukeni kwamba mnatakiwa kurejesha mkopo kwa wakati ili tuendelee kuwakopesha wajasirimali wengine”, alisema Mshaweji.


Kwa upande wake Ofisa maendeleo ya jamii wa Manispaa ya Songea, Naftali Saiyoloi alisema kuwa mkopo huo umetolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana ikiwa ni lengo la kuinua hali zao kiuchumi katika makundi hayo mawili na kwamba aliongeza kuwa, mfuko wa kukopesha wanawake na vijana ulianzishwa mwaka 1993 ukilenga kuongeza ajira na kuinua uchumi wa mwananchi wa kawaida.

No comments: