Baadhi ya watoto wenye ulemavu (Albino) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa halmashauri ya mji wa Mbinga. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wa
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa kuacha tabia ya kuwafungia ndani
ya nyumba zao watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali badala yake wajenge
mazoea ya kuwafichua watu wenye tabia ya kuwaficha watoto hao, ili waweze
kupata haki zao za msingi.
Aidha
wameshauriwa kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye walemavu ikiwemo
unyanyasaji, ubaguzi na kwamba wanapaswa kujenga mazoea ya kuwapenda, kuwajali
na kuwahudumia ipasavyo kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana matatizo ya
viungo.
Diwani wa
viti maalumu kata ya Ruanda, Imakulatha Mapunda alisema hayo juzi alipokuwa
akifungua mafunzo ya siku mbili ya sheria ya watu wenye ulemavu, yaliyofanyika
katika kata hiyo wilaya ya Mbinga mkoani hapa ambayo yalifadhiliwa na shirika
lisilokuwa la serikali la The Foundation for Civil Society.
“Ndugu zangu
tunapaswa kuwa wasikilizaji wazuri katika mafunzo haya, huko tuendako
tukayatumie vyema kwa kuyafikisha kwa wengine ambao hawakubahatika kuhudhuria
hapa ili waweze kutambua haki zao za msingi”, alisisitiza Mapunda.
Naye Henry
Digongwa ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka idara ya maendeleo ya
jamii wilayani humo alifafanua kuwa, mambo yanayokwamisha kutotekelezeka kwa
haki za watu wenye ulemavu ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoteua Mwenyekiti wa
taifa wa baraza la watu wenye walemavu, ambaye angeweza kusimamia masuala
mbalimbali ya kundi hilo tete.
Digongwa
alifafanua pia vikwazo vingine vinavyorudisha nyuma maendeleo ya watu hao ni
kutoteuliwa kwa Waziri mwenye dhamana na Wajumbe watakaowakilisha watu wenye
ulemavu, katika baraza la walemavu taifa na serikali kuwa na mifumo ya kutenga
bajeti ndogo ya kuhudumia watu hao ambayo haikidhi mahitaji husika.
Pia aliongeza
kuwa inapaswa kuunda Kamati ndogo za kuhudumia walemavu kutoka ngazi ya mtaa,
wilaya, mkoa mpaka taifa ambayo itasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Vilevile Amos
Komba ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya mwanzo wilaya ya Mbinga, alisisitiza kuwa
mlemavu yeyote yule anatafsiriwa kuwa ni binadamu mwenye haki sawa kama
walivyokuwa watu wengine ambao hawana ulemavu hivyo anastahili kupata haki zote
za msingi kama watu wengine.
Komba alisema
kuwa pale watoto wenye ulemavu wanaponyanyaswa kwa namna moja au nyingine, mtu
yeyote sheria inamruhusu kutoa malalamiko kwa Kamati ya maofisa wa ustawi wa
jamii au kwenda kushtaki Mahakamani kufungua mashtaka dhidi ya kosa aliloliona
linafanyika.
No comments:
Post a Comment