Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
JUMLA ya Kaya saba zenye wakazi zaidi ya 40 waishio katika
kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamekosa mahali pa kuishi
kutokana na nyumba zao kuezuliwa na mvua kubwa ambayo iliambatana na upepo
mkali.
Tukio hilo lilitokea Novemba Mosi mwaka huu majira ya saa 11
jioni katika kata hiyo, huku wengine baadhi yao nyumba zao zikiwa zimenusurika
kubomolewa baada ya kuezuliwa na upepo huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas
Nshenye alisema kuwa jumla ya nyumba 32 za wananchi ziliezuliwa na upepo huo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge ambaye
alitembelea katika eneo la tukio hilo Novemba 8 mwaka huu akiwa ameambatana na
waandishi wa habari, alisikitishwa na uongozi wa wilaya hiyo kwa kuchelewesha
kutoa taarifa ya tukio hilo ambapo alikemea hali hiyo na kutaka isijirudie
tena.
Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Ruvuma ikiongozwa na
Mwenyekiti wake Dkt. Mahenge baada ya kupata taarifa za tukio hilo, kutoka kwa
wasamaria wema ilichukua jukumu la kutembelea wananchi hao waliokumbwa na maafa
hayo.
“Nimesikitishwa sana na kitendo cha viongozi wa wilaya hii
kuchelewesha taarifa za tukio hili ofisini kwangu, hawa watu wamepatwa na maafa
siku kadhaa zilizopita wanahitaji kupatiwa msaada”, alisema Dkt. Mahenge.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema kuwa katika
nyumba hizo 32 za wananchi zilizoezuliwa, nyumba tatu ni za taasisi za umma
ikiwemo ofisi ya Kata, Mahakama ya mwanzo na kwamba hadi sasa kaya saba hazina
uwezo wa kuezeka tena nyumba zao huku tathimini ya awali ikionesha kwamba
wamepata hasara ya milioni 14.
Nao kwa upande wao baadhi ya wananchi waliokumbwa na maafa
hayo wakizungumza kwa nyakati tofauti, wameiomba serikali kuangalia uwezekano
wa kuwasaidia haraka kwani hawana mahala hata pa kulala.
Hata hivyo baada ya kutembelea waathirika wa tukio hilo, Mkuu
wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge pamoja na kuahidi kusaidia wananchi hao baada
ya tathimini kukamilika, lakini pia amesisitiza ujengaji wa nyumba imara za
kisasa ili waweze kuepukana na majanga kama hayo ambayo yanaweza kujitokeza
tena hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment