Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera akisisitiza jambo katika mikutano yake ya hadhara wilayani hapa hivi karibuni. |
Na Muhidin Amri,
Tunduru.
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera
amewataka wananchi wa wilaya hiyo kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli kwa
kujikita zaidi katika kufanya kazi za kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao
badala ya kutumia muda wao mwingi, kupiga porojo za kisiasa ambazo zimeshapita
muda wake.
Aidha Homera, amewahimiza kuanza maandalizi ya msimu mpya wa
kilimo wakati serikali nayo ikijiandaa kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji
wa pembejeo za kilimo, jambo ambalo litasaidia kuongeza uzalishaji mashambani.
Ametaoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa katika ziara
yake ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo katika vijiji mbalimbali vya
kata ya Malumba, Nakapanya, Nandembo na Mpanji wakati akikagua pia zoezi la
ufyatuaji tofari kwa kila kijiji wilayani humo.
Pia Mkuu huyo wa wilaya, alitembelea shule ya sekondari
Nandembo ambapo aliwakumbusha wanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyo kusoma
kwa bidii na kuwa wazalendo katika nchi yao, kama alivyosisitiza Baba wa taifa
hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake.
Mbali na hilo, alikutana pia na vikundi vya wanawake na vijana
waliojiunga kwenye vikundi vya Vicoba na kuwataka makundi mengine ya kijamii
hususani wakulima nao kuunda vyama vya akiba na mikopo, ili waweze kujikwamua
kiuchumi.
Kutokana na hilo Mkuu wa wilaya, Homera alisema kuwa wananchi
hao watakaojiunga katika vikundi hivyo serikali ipo tayari kuwaunga mkono kwa
namna moja au nyingine ili waweze kusonga mbele kimaendeleo na hatimaye waweze
kuondokana na umaskini.
No comments:
Post a Comment