Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WATU wawili ambao ni wakazi wanaoishi katika kijiji cha
Mbwambwa kata ya Mpitimbi wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, wamefariki dunia
baada ya kuungua moto waliokuwa wameuwasha wakati wakiwa wanawinda porini.
Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa
mkoa huo Zubery Mwombeji aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Athuman Hashim
(16) na Said Liugu (27) wote wakazi wa kijiji hicho.
Mwombeji alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 9 mwaka
huu majira ya saa 7 mchana ambapo Hashim na Liugu ambao wamekuwa
wakijishughulisha na uwindaji walienda bondeni kwenye kijiji hicho ambako
walichoma moto pori walilokuwa wakiwinda, kwa lengo la kutaka kuwaona kwa
urahisi wanyama aina ya Ndezi ambao walikuwa wakiwawinda.
Alibainisha kuwa wawindaji hao baada ya kuwasha moto huo
ambao baadaye ulionekana kuwashinda, uliwaka sehemu zote ukiwa umewazunguka na
kusababisha washindwe mahali pa kukimbilia kwa sababu hata maeneo ya njia ya
kurudia wao, moto ulikuwa umewazingira na kusababisha washindwe kujiokoa hadi
mauti yalipowakuta.
Vilevile alieleza kuwa watu waliokuwa jirani na eneo hilo
walipoona moto mkubwa ukisambaa hovyo walikwenda kwenye eneo la tukio kusaidia
namna ya kuuzima lakini ilishindikana na baadaye uongozi wa serikali ya
kijiji hicho, kwa kushirikiana na wananchi walipokwenda kwenye eneo la tukio
hilo kwa lengo la kuuzima pia nao walishindwa.
Alisema kuwa baadaye moto ulipopungua ndipo waliiona miili ya
watu wawili wakiwa wameungua moto ambao baadaye walifahamika kuwa
ni Hashim na Liugu ambao walikuwa wakijishughulisha na kazi hiyo ya
uwindaji.
Kadhalika Polisi walipopewa taarifa kuhusiana na tukio hilo,
waliwasili katika eneo la tukio huku wakiwa wameongozana na mganga kutoka kituo
cha afya Mpitimbi ambaye alithibitisha kuwa watu hao tayari walikuwa wamekufa
kutokana na kuungua moto.
Pia ndugu wa marehemu hao waliwasili nao kwa ajili ya
kuchukua miili hiyo kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Hata hivyo katika tukio jingine jeshi la Polisi mkoani Ruvuma
limefanikiwa kuwakamata watu wawili Yassin Yassin (44) mkazi wa kijiji cha
Mchomoro na Mussa Sandari (70) mkazi wa kijiji cha
Ligela wilayani Namtumbo mkoani hapa, wakiwa na misokoto ya bhangi
gramu 250 na miche ya bhangi 99 iliyokuwa imepandwa katikati ya shamba la
mahindi lililopo kwenye hifadhi ya wanyama ya Mbalanga wilayani humo.
No comments:
Post a Comment