Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
MKUU wa wilaya ya Tunduru Juma Homera, ameliagiza Jeshi la
Polisi wilayani hapa kuhakikisha kwamba linawakamata na kuwafikisha Mahakamani
baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mbati ambao wanaojihusisha na utengenezaji na
uuzaji wa pombe haramu aina ya gongo.
Pia ametoa siku tatu kwa serikali ya kijiji hicho viongozi
wake kwenda ofisini kwake kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu
kutokana na kuwepo kwa wanananchi, wanaovunja sheria za nchi hivyo kukwamisha
juhudi za serikali katika kupambana na vitendo vya uhalifu ambavyo vinachangia
kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Homera alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, wakati alipokuwa
akizungumza katika mkutano wa hadhara ambapo aliwataka wakazi wa kijiji hicho
kuwafichua wale wote ambao wamekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali,
ikiwemo kazi ya ufyatuaji tofali 100,000 kwa kila kijiji agizo ambalo lilitolewa
na Rais Dkt. John Magufuli.
Kadhalika kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa kugombea ardhi
kati ya kijiji hicho cha Mbati na kijiji jirani cha Mdabwa ambao umekuwa
ukisababishwa na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mbati kutokana na muda mwingi
hujihusisha na matumizi ya unywaji wa pombe ya gongo na kushindwa kuzuia
hisia zao pale wanapokunywa jambo ambalo linachangia kuchelewesha maendeleo
katika vijiji hivyo vyote viwili.
Kutokana na hali hiyo Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza viongozi
wa vijiji hivyo kwenda ofisi ya halmashauri ya wilaya hiyo kupitia idara yake
ya ardhi, kumaliza suala hilo la migogoro ya mipaka ya ardhi ambalo linachangia
wananchi washindwe kufanya shughuli zao za maendeleo.
Katika hatua nyingine Ofisa mtendaji wa kijiji cha Mbati
Halid Maridad, anatuhumiwa kutafuna fedha shilingi milioni 1.5 ambazo zilichangwa
na wakazi wa kijiji hicho kwa ajili ya utengenezaji wa madawati.
Kijiji hicho ni kati ya vijiji vitatu vinavyounda kata ya
Mbati ambavyo bado vipo nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na vijiji vingine katika
wilaya ya Tunduru.
Ofisa mtendaji huyo anadaiwa kutokomea
kusikojulikana baada ya kusikia kwamba Mkuu wa wilaya, Homera na Kamati ya
ulinzi na usalama ya wilaya hiyo inakwenda kijijini
hapo kwa ajili ya kupata taarifa kamili juu tukio hilo.
Homera ametao siku tatu kwa Ofisa mtendaji huyo kujisalimisha
ofisini kwake popote pale alipo ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya matumizi ya
fedha hizo ambazo zilikusudiwa kukamilisha utengenezaji wa madawati ya kukalia
wanafunzi.
No comments:
Post a Comment