Na Gideon Mwakanosya,
Songea.
HALMASHAURI Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imevuka lengo
la utoaji chanjo kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano na kufikia
asilimia 217.5 katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.
Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alimweleza
mwandishi wetu kuwa katika kutekeleza zoezi hilo la chanjo ya kitaifa kwa
kuhakikisha kila mtoto anafikiwa, limeweza kuleta ufanisi mkubwa kwa kukidhi
vigezo vya utoaji chanjo ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yale yanayozuiliwa
kwa chanjo.
“Manispaa yetu imevuka lengo hili kutokana na watoto na akina
mama wajawazito kutoka nje ya halmashauri, kupata huduma katika vituo vyetu vya
kutolea huduma za afya”, alisema.
Alivitaja vituo hivyo ambavyo vinatumika kwa kufanya kazi
hiyo kuwa ni hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma, kituo cha afya Mjimwema na
Mshangano, zahanati ya Matarawe, Mtakatifu Norbert, Bombambili na Tanga vyote vilivyopo
mjini hapa.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dkt. Simon Chacha alitoa
wito kwa wazazi na walezi wote kuhakikisha kwamba mtoto yeyote mwenye umri
chini ya miaka mitano afikishwe katika kituo husika cha kutolea huduma ili kukamilisha
chanjo kulingana na ratiba husika za uchanjaji.
Kulingana na takwimu za kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu, Manispaa
hiyo ina jumla ya wakazi 220,932 kati yao watoto chini ya mwaka mmoja ni 8175, watoto
chini ya miaka mitano ni 37,559 na akina mama wajawazito ni 8,837.
Manispaa ya Songea ina jumla ya vituo 31 vya kutolea huduma
ya afya kati ya hivyo kuna hospitali moja, vituo vya afya vinne na zahanati 26
huku vituo vinavyotoa huduma za chanjo vikiwa jumla yake ni 26 kati ya hivyo
vituo vitano ni vya watu binafsi.
No comments:
Post a Comment