Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
ameonesha kuchukizwa kwake na tabia kwa baadhi ya watendaji wa serikali
wilayani humo wanaoshindwa kusimamia kikamilifu sheria zilizopo hatua
ambayo huchangia kwa namna moja au nyingine, wananchi wazivunje kwa kukataa
kutii maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa serikali.
Cosmas Nshenye. |
Nshenye alitolea mfano kwa agizo la serikali kuzuia uuzaji na
unywaji wa pombe saa za kazi, hata hivyo mamlaka zinazohusika kusimamia
hilo kama vile jeshi la Polisi na halmashauri kupitia kitengo chake cha
biashara wahusika wamekuwa wakikaa kimya bila kuchukua hatua.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza maafisa biashara
wa halmashauri ya wilaya na mji wa Mbinga, kuwakamata na kuwapiga faini au
kuwafutia leseni wale wote wanaofanyabiashara ya kuuza pombe saa za kazi.
Alitoa agizo hilo hivi karibuni alipokuwa akitoa salamu za
serikali katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga,
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.
Nshenye aliwataka pia watumishi wa umma kutimiza wajibu wao ipasavyo
pasipo kusubiri kusukumwa kwani ni kosa kwa mtumishi wa
serikali kushindwa kuleta tija eneo lake la kazi kwani serikali ya awamu ya
tano, tangu ilipoingia madarakani imedhamiria kuleta mabadiliko makubwa kwa
Watanzania ikiwemo kuboresha huduma za kijamii na maisha bora kwa wananchi wake
kwa kuwapatia huduma zilizokuwa bora.
Alisema kuwa kwa mtumishi asiyetaka kubadilika kwa kuongeza
uwajibikaji mzuri mahali pake pa kazi ni vyema akatafuta kazi nyingine ya
kufanya au kwenda wilaya nyingine, lakini sio kubaki Mbinga ambayo imekuwa
na historia nzuri ya wananchi wake kupenda kujituma kufanya kazi za kujiletea
maendeleo bila kusukumwa.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kutunza afya za
binadamu kwani itazuia hatari ya binadamu kupata magonjwa mbalimbali
ambayo yanatokana na kunywa maji machafu ambayo huchafuliwa kwa takataka wakati
wa kuosha magari kwenye vyanzo hivyo.
“Kazi hizi za kuosha magari zifanywe katika maeneo maalumu
yaliyotengwa na kujengwa ‘Car wash’ ili hata halmashauri iweze kukusanya mapato
yake, badala ya kufanywa katika maeneo ambayo sio rasmi”, alisisitiza Nshenye.
Vilevile amemtaka Ofisa mazingira wa halmashauri ya mji wa
Mbinga kusimamia jambo hilo kwa kuhakikisha wale wote waliopo katika maeneo ya
vyanzo vya maji wanaondolewa haraka kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment