Joseph Fuime akiwa katika majukwaa ya mikutano ya siasa mjini Songea iliyofanyika hivi karibuni. |
Na Gideon Mwakanosya,
Songea.
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya
Songea mkoani Ruvuma, kimemvua uanachama Joseph Fuime akidaiwa kufanya makosa
mbalimbali ikiwemo kukihujumu chama hicho wakati alipokuwa mgombea ubunge kupitia
tiketi ya CHADEMA jimbo la Songea mjini, katika uchaguzi mkuu uliopita Oktoba
25 mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisini kwake, Katibu
wa CHADEMA wilaya ya Songea, Olais Ng`ohison alisema kuwa Fuime amefutwa kwenye
orodha ya kuwa mwanachama wa chama hicho, tangu Octoba 23 mwaka huu na
kwamba hivi sasa sio mwanachama tena wa chama hicho.
Alisema kuwa chama hicho kimelazimika kutoa taarifa
kupitia vyombo vya habari kuwajuza wananchi, wadau, wakereketwa pamoja na
viongozi mbalimbali wa serikali baada ya kubaini kwamba watu wengi walikuwa
hawafahamu kuondolewa na kufutwa uanachama kwa Fuime.
Kadhalika alifafanua kuwa Fuime katika kipindi cha
uchaguzi mkuu wa mwaka jana alikuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho,
lakini alikihujumu chama kwa mambo mbalimbali yakiwemo ya kutoshiriki katika
majumuisho ya kura kwenye ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Songea na kuamua
kuzima simu zake zote za kiganjani bila sababu za msingi.
Kutokana na hali hiyo alisema amesababisha kuathiri
ruzuku ya chama katika ngazi zote kutokana na udanganyifu wa kura alioufanya na
kwamba alipoandikiwa na chama hakuweza kujibu na alikataa kufika kwenye
kikao cha kamati tendaji ambacho kilitaka kumhoji juu ya tuhuma hizo na aweze
kuzitolea ufafanuzi wa kina.
Alisema kwamba kufuatia hujuma hizo kamati tendaji ya Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo wilaya ya Songea imeamua kumfukuza uanachama Fuime huku
chama kikiwataka wadau wake wote kutoshirikiana naye katika maswala yoyote
yanayohusu chama hicho ndani na nje ya wilaya ya songea.
Kwa upande wa waandishi wa habari walipofanya
mawasiliano na Joseph Fuime na kumtaka atoe ufafanuzi juu ya kufukuzwa kwake
kwenye chama hicho alisema kuwa hatambui juu ya kufukuzwa huko, bali
anachofahamu yeye ni bado mwanachama wa CHADEMA huku akiongeza kuwa kadi yake
ya uanachama ameilipia hadi mwaka 2020 ambayo bado anaendelea kuimiliki.
No comments:
Post a Comment