Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
wamelalamikia kuwepo kwa tatizo kubwa la upungufu wa madawa na vifaa tiba
katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo wilayani humo, jambo ambalo
linawafanya wagonjwa wengi washindwe kupatiwa matibabu.
Baadhi yao walisema kuwa licha ya kusikia matangazo kupitia
vyombo vya habari kutoka kwa Waziri mwenye dhamana kwamba hakuna tatizo la
upungufu wa madawa katika hospitali na vituo hivyo vya afya hapa nchini, hali hiyo imekuwa
kinyume ndani ya wilaya hiyo ambapo maeneo mengi wagonjwa wanashindwa kupatiwa
matibabu kutokana na kukosekana kwa madawa hayo.
Walifafanua kuwa hata kwa upande wa wanachama wa Mfuko wa
bima ya afya (CHF) wengi wao hawapatiwi matibabu ipasavyo kutokana na sehemu
ambako wanatolea huduma za afya kutokuwepo kwa madawa na vifaa tiba, jambo
ambalo Madiwani katika kata zao wanashindwa kuendelea kuhamasisha wananchi wao
waendelee kuchangia mfuko huo.
Hayo yalisemwa na Madiwani hao katika kikao chao cha baraza
kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa na kuongeza kuwa, tatizo
hilo sasa limekuwa sugu hivyo kuna kila sababu ya kulitafutia ufumbuzi wa
haraka ili kuweza kumaliza kero hiyo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti sisi katika maeneo yetu hivi sasa
tunashindwa hata kuhamasisha hawa wananchi kuendelea kuchangia katika mfuko huu
wa bima ya afya, tunapokuwa kwenye mikutano pale tunapozungumzia suala hili
tunazomewa na kuambiwa kwamba hata pale wanapochangia fedha zao hawapatiwi
matibabu, hivyo tunaitaka serikali ione namna ya kuweka sawa jambo hili”,
alisema Kelvin Kapinga diwani kata ya Nyoni.
Kwa upande wake akijibu hoja hiyo iliyotolewa na madiwani hao
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Vivian Mndolwa alieleza
kuwa tayari kuna baadhi ya dawa zimeletwa na bohari kuu ya madawa ambapo
zitaanza kusambazwa hivi karibuni ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment